Lugha, Fasihi na Elimu

GWIJI WA WIKI: Otieno Mjomba

January 4th, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

MBINU rahisi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa masomo miongoni mwa wanafunzi ni kuwaaminisha kwamba hakuna lisilowekezana chini ya jua.

Pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo husisimua wanafunzi, matumizi ya video, michoro na picha za rangi ni namna nyingine ya kufanya masomo kuwa ya kuvutia.

Haya ni kwa mujibu wa mwalimu Otieno Mjomba ambaye sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya St Jude Donholm jijini Nairobi.

“Matumizi ya mbinu za ufundishaji zinazohusisha ubunifu wa kiteknolojia hupanua mawanda ya fikira za wanafunzi na kuwachochea kuwa wavumbuzi. Huu ni mwaka mwingine utakaoshuhudia mabadiliko mengi kiteknolojia. Walimu tuyakumbatie mageuzi hayo ili kurahisisha kufaulu kwa wanafunzi katika safari zao za elimu. Ni mwaka wa kila mwalimu kuenda na wakati na majira. Usibaki nyuma kukwamia kipande cha kijiti cha jana katika bahari iliyo na vyuma na kamba za kisasa za kuboresha uogeleaji wako hadi ukafikia ufuo wa ufanisi,” anashauri.

Mjomba alizaliwa miongo mitatu na nusu iliyopita katika kijiji cha Kanyaudo, Kaunti ya Siaya. Alisomea katika shule za msingi za Kanyaudo na Nyalenya kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya St Paul’s Ndenga (Siaya) kisha Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha International Teaching & Training Centre (ITTC), Dagoretti (2006-2008).

Ana digrii ya mawasiliano na mahusiano ya umma kutoka Chuo Kikuu cha Moi (2018-2022) na sasa anasomea shahada ya uzamili katika masuala ya mawasiliano chuoni humo.

Baada ya kuhitimu ualimu mnamo 2008, Mjomba alianza kufundisha katika Shule ya Summit Vine Academy iliyoko Kaunti ya Kiambu kabla ya kuhamia Acacia Green Academy (Kiambu) kisha Junel Academy, Nairobi.

Aliwahi pia kufundisha katika shule za Jubilant Junior (Ruai) na Rockfields Junior (Nairobi).

Alijiunga na St Jude Doonholm mnamo 2020 na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili kisha Mratibu wa Mipango (2024).

Zaidi ya ualimu, Mjomba pia ni mwandishi wa vitabu na mshauri nasaha katika kampuni ya Niken Marketing and Communications Ltd jijini Nairobi.

Kampuni hiyo inayotoa ushauri nasaha kwa wanafunzi na walimu, pia hushughulikia uundaji wa mipango mikakati ya mashirika mbalimbali pamoja na kuandaa sherehe na tafrija za kila sampuli katika kiwango cha mtu binafsi, kundi la watu, kampuni au shirika.

Baadhi ya vitabu vyake ni ‘Fumbuo la Insha’, ‘Fumbuo la Msamiati’ na novela ya Kiingereza ‘Sour Grape’ inayopatikana kwenye Amazon.com.

Amechapishiwa pia hadithi fupi ‘Fundo la Moyoni’ katika antholojia ‘Boda Mpya na Hadithi Nyingine’.

Ana miswada mingi ya riwaya na hadithi ambayo ingali katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika kampuni na mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu humu nchini.

Mjomba pia ni mtaalamu wa elimu ambaye hushiriki mahojiano na mijadala ya kitaaluma kupitia mitandao, redio na runinga za humu nchini huku akiandika makala ya elimu na siasa katika gazeti la ‘Daily Nation’.

Kwa kutumia kipaji chake cha uandishi, amepiga hatua kubwa katika ufundishaji kutokana na upekee wa kuoanisha talanta, ujuzi wa kiteknolojia na taaluma alizozisomea.

Mjomba hupeperusha vipindi anuwai vya kuasa, kuchanganua na kuhakiki masuala yanayoathiri mtoto wa Kiafrika katika jamii kupitia jukwaa la ‘Paukwa Radio Podcast’.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa miongoni mwa walimu watakaobadilisha sura ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kiteknolojia katika enzi hizi za utandawazi.

Baadhi ya wanafunzi wake ni waigizaji wa kizazi kipya – Baha (Tyler Mbaya) na Stella (Natasha Ngegie) – katika mchezo wa runingani ‘Machachari’.