Makala

GWIJI WA WIKI: Paskali Watua

November 25th, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

WENGI wetu huona shida ikiwa na uhasi katika maisha ya mwanadamu.

Hata hivyo, shida ndizo humfanya mtu kuwa mbunifu nao ubunifu ukamfanya mwanadamu aanze kusowerea katika njia ya mafanikio.

Mafanikio nayo huhitaji matumaini na uvumilivu. Bidii, matumaini na stahamala huoana na huhitajiana ili mtu afaulu katika chochote anachokifanya.

Japo tumeaminishwa kuwa bidii na kujituma ni kati ya mambo yanayochangia mafanikio, dhana hii ina ukweli tatanishi kwani, mafanikio ni ubunifu tu unaohitaji akili nyingi na nguvu kiasi. Au wewe, hapo ulipo, umewahi kumwona punda aliyefanikiwa?

Aidha, si kwamba mafanikio huja kama ajali. La hasha! Kati ya vitu vilivyo na uwezo wa kumfaulisha mtu au kumzuia asifanikiwe kabisa, ni fikra zake! Fikra hasi huzaa hasara nazo fikra chanya huzaa ubora. Fikra ni kama mbegu inayopandwa gizani na ikaota mchana wa jua! Hivyo, maisha anayoishi mtu, huwa ni zao la mawazo yake.

Usikate tamaa! Wewe unayepania kufanikiwa, jambo muhimu kwako ni kudumisha matumaini, kujiwekea malengo na kuruhusu fikra chanya zitawale ndani ya ubongo wako. Ukiwa unaazimia kufaulu, ni busara kujenga taswira ya mafanikio yako kwenye fikra na kuyatazama kila leo kwa darubini ya akili kichwani mwako.

Iwapo mafanikio yangekuwa mepesi jinsi baadhi yetu tunavyoyachukulia, basi kufaulu kusingekuwa na maana yoyote!

Huu ndio ushauri wa Bw Paskali Null Watua almaarufu Mwanafalsafa – mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa anasomea Teknolojia ya Mawasiliano nchini Ireland.

MAISHA YA AWALI

Paskali alizaliwa mnamo Februari 16, 1996, katika kijiji cha Matuguta, kata ya Githiga, kaunti ndogo ya Githunguri, gatuzi la Kiambu. Yeye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano wa Bw Stephen Watua na Bi Beatrice Watua. Nduguze Paskali ni Irene Nafuna Watua, Thomas Wadabwa Watua, Jackline Nandudu Watua na Susan Kainza Watua.

Paskali alianza kuhudhuria masomo ya chekechea mnamo 2001 katika Shule Msingi ya Githiga Centre Junior Academy ambayo kwa sasa inaitwa PCEA Githiga Academy, Kaunti ya Kiambu.

Baada ya kusoma kwa kipindi cha mwaka mmoja, alijiunga tena na chekechea ya Shule ya Msingi ya Matuguta, Kiambu mnamo 2002. Alisomea huko kwa miaka miwili kabla ya kujiunga na Darasa la Kwanza katika shule hiyo hiyo.

Paskali alifanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo 2011 na akawa miongoni mwa watahiniwa bora kutoka Shule ya Msingi ya Matuguta na eneo pana la Githunguri.

Ingawa aliitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Gathiruini, Kiambu, uchechefu wa karo ulimnyima nafasi ya kusomea katika shule hiyo maarufu na akalazimika kujiunga na shule ya kutwa ya Gikang’a Kagece, Kiambu mnamo 2012.

Mnamo 2014, aliteuliwa kuwa Naibu Kiranja Mkuu wa maktaba ya shule. Ni katika mwaka huo ambapo alijumuishwa katika kundi la wanafunzi walioshiriki mashindano ya somo la Hisabati katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Githiga, Kiambu.

Aliibuka miongoni mwa wanafunzi bora na akateuliwa kuhudhuria kongamano la wanafunzi katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance, Kikuyu.

Paskali alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2015 na akawa wa pili katika orodha ya mwa watahiniwa waliotia fora zaidi kutoka Shule ya Upili ya Gikang’a Kagece.

Baada ya hapo, aliajiriwa katika duka la jumla jijini Nairobi kabla ya kujiunga na Chuo cha Teknolojia cha Murang’a mnamo 2016. Baada ya mwaka mmoja, safari yake ya masomo ilikatika ghafla kutokana na hali ya mbaya ya kiuchumi ya wazazi wake. Hata hivyo, hakukata tamaa.

Mnamo 2019, Paskali alijiunga na Chuo cha Microsoft Training Academy (MTA) kuendeleza kozi yake ya Teknolojia na Mawasiliano. Kwa sasa, anasoma kwa njia ya mtandao katika chuo hicho cha MTA kilichoko nchini Ireland.

UANDISHI

Zaidi ya kuwa mwanafunzi wa Teknolojia na Mawasiliano, Paskali ni mwandishi wa kazi za kibunifu kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Ingawa kipaji cha uandishi kilianza kujikuza ndani yake akiwa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu mnamo 2014, aliyemchochea zaidi kujitosa katika ulingo wa sanaa ya utunzi ni mwandishi chipukizi raia wa Tanzania, Lovi Pius Kijogoo.

Paskali alianza kwa kuandika mashairi, simulizi na nudhuma za kimapenzi mnamo 2018 huku akizipakia kwenye makundi ya mtandaoni yanayomilikiwa na watunzi wa Tanzania.

Mwaka uo huo, aliandika riwaya mbili – ‘Ngumu Kuelewa’ na ‘Mwisho wa Mwanzo’ ambazo anatazamia zitachapishwa mwaka huu. Paskali pia ameshirikishwa katika utunzi wa mikusanyiko mbalimbali ya hadithi fupi.

Hadithi yake ‘Jinamizi la Uhuru’ ilichapishwa na kampuni ya The Writers’ Pen Publishers, Eldoret katika mkusanyiko wa ‘Shaka ya Maisha na Hadithi Nyingine’ mnamo Julai 2020.

Paskali ndiye mwandishi wa hadithi ‘Kauli ya Mwisho’ katika mkusanyiko wa ‘Harusi ya Kiharusi na Hadithi Nyingine’ uliofyatuliwa na kampuni ya Bestar Publishers mnamo Julai 2020.

Kampuni ya African Ink Publishers imemtolea pia hadithi ‘Shani ya Kiama’ katika mkusanyiko wa ‘Maskini Maarufu na Hadithi Nyingine’ na hadithi ‘Panya Mlafi’ katika antholojia ya ‘Kasuku wa Salome na Hadithi Nyingine’ mnamo Agosti, 2020.

Baadhi ya mashairi yake yamejumuishwa katika ‘Diwani ya Maradhi’ iliyochapishwa na The Writers’ Pen mnamo Agosti 2020.

Kwa sasa anatazamia kampuni ya African Ink imchapishie hadithi ‘Takbiri’ na ‘Samahani Mke Wangu’ katika antholojia ya ‘Mapenzi ya Mwanaharamu na Hadithi Nyingine’ wakati wowote kuanzia sasa.

Paskali amechangia pia mashairi ya Kiingereza katika diwani ya ‘When I Marry Rimanto’ (The Writers’ Pen, Julai 2020) na ‘Shackles Of Pain’ (The Writers Pen, Februari 2020). Zaidi ya hayo, ameandika diwani ya mashairi ya Kiingereza kwa jina ‘Games Of Witches’ iliyochapishwa na Elong’o Publishers mnamo Machi 2019.

Baadhi ya kazi za Paskali zimejumuishwa katika majarida mbalimbali nchini likiwemo Jarida la The Writers’ Pen. Amepokea vyeti na tuzo kadhaa za haiba kubwa kutokana na uandishi wake wa mashairi ya Kiingereza.

Paskali anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali.

Anamstahi pakubwa mkewe Bi Rosa Nyaboke ambaye amekuwa nguzo muhimu katika juhudi zake za kuchapukia sanaa ya uandishi. Kwa pamoja, wamejaliwa mtoto wa kike – Elora Beatrice Watua.

Ni naima kwa Paskali kujumuishwa kati ya magalacha wa kazi za fasihi. Lengo lake kuu ni kushirikiana na wenzake katika kundi la Writers Unity kuwalea na kuwakuza chipukizi wanaoibukia katika uandishi wa kazi bunilizi na kuwashirikisha katika mashindano mbalimbali ya fasihi.