Makala

GWIJI WA WIKI: Richard Mwangi Mbugua

December 4th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUFANIKIWA maishani na kitaaluma kunamhitaji mtu kuwa na bidii, unyenyekevu, stahamala na heshima ambayo si utumwa.

Kuvuta subira katika kila jambo unalolishughulikia ni sifa nyingine itakayokufungulia milango ya heri.

Mara nyingine, mja anaweza kuteseka hata kama amesoma hadi kufikia viwango vya juu vya kuenziwa. Katika hali hii, si vyema kabisa kukata tamaa. Badala yake, mtu hutakiwa kuyaelekeza macho yake kwa Mola ambaye ni mpaji wa kila kitu.

Kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila jambo unalolitenda ni mwanzo wa tabasuri. Kwa kuwa Mungu alikuumba kwa mfano wake mwenyewe, unatakiwa siku zote kumuamini katika kila hatua unayoipiga kusonga mbele.

Huu ndiyo ushauri wa Bw Richard Mwangi Mbugua; mwandishi chipukizi ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Kijabe Integrity.

Maisha ya awali

Bw Mbugua alizaliwa mnamo Septemba 15, 1992, katika kijiji cha Kisa, eneo la Webuye, Kaunti ya Bungoma akiwa mtoto wa tatu wa marehemu Mzee Yohana Wanjala na Bi Leah Muthoni. Alilelewa katika kitongoji cha Omusalaba, viungani mwa mji wa Bungoma. Ni hadi mwaka wa 1996 ambapo walihamia katika eneo la Kimende; kisha Kirenga katika Kaunti ya Kiambu.

Alianza rasmi safari yake ya masomo mnamo 1999 alipojiunga na Shule ya Chekechea ya Kirenga. Mnamo 2002, alijiunga na Shule ya Msingi ya Kirenga akiwa mwanafunzi wa Darasa la Kwanza. Alisomea huko hadi mwaka wa 2009 na kufaulu vyema kwa kuibuka mwanafunzi wa pili bora katika mtihani wa KCPE.

Mnamo 2010, alijiunga na Shule ya Upili ya Nyahururu, Kaunti ya Nyandarua. Alisomea huko kwa kipindi cha miaka miwili pekee kabla ya aliyekuwa akiyafadhili masomo yake kusitisha ghafla msaada aliokuwa akimpokeza baada ya kukumbwa na janga ambalo nusura limfilisishe kabisa.

Kwa kweli, mti mkuu ukigwa wana wa nyuni huyumba! Ingawa changamoto za kila sampuli zilitishia kuuzima kabisa mshumaa wa tumaini lake la kukamilisha masomo ya sekondari, Mbugua aliamini kuwa dau la mnyonge haliendi joshi.

Ilimjuzu kuanza kujishughulisha na biashara ndogondogo pamoja na kufanya uhamali na vibarua vingine vya kila sampuli ili apate karo ya kujiendeleza kielimu.

Bahati ni kama ajali na haijulikani ijapo. Baada ya kufanya vibarua vya kijungu-jiko na kazi nyingi za sulubu na shokoa, Mbugua alibahatika kukutana na msamaria mwema aliyemsaidia kwa kumlipia karo ya kujiunga na Shule ya Upili Nyamweru, Kiambu mnamo 2012 akiwa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu.

Katika muhula wa pili, mambo yake yakaanza tena kuenda kama hapo mwanzoni. Aliachwa bila mtu yeyote wa kumlipia karo. Alienda shuleni akitembea peke bila viatu, bila kisebeho, chamcha au chajio.

Kwake, maisha yalielekea kukosa maana, yakawa bure mithili ya kaka tupu la yai. Ingawa hivyo, hakupoteza tumaini la kuishi. Aliendelea kujikaza kisabuni; akijikusuru, kujihini na kujihimu.

Baada ya kuufanya mtihani wake wa mwisho wa Kidato cha Nne (KCSE) na kupita vizuri, uchechefu wa fedha haukumwezesha kujiunga na chuo kikuu. Aliendelea kutarazaki, akitumainia kupata hela za kujiunga na chuo kikuu siku moja ili asomee ama ualimu au uanahabari. Hizi ni taaluma ambazo Mbugua alivutiwa kwazo tangu akiwa mwanafunzi wa Darasa la Nne shuleni Kirenga. Mungu hamwachi mja wake.

Mbugua alifaulu kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania mnamo 2015 kusomea Kiswahili (Isimujamii) na Lugha nyingine za Kiafrika.

Ualimu

Baada ya kukamilisha mtihani wake wa KCSE mnamo 2013, Mbugua alipata kibarua cha kufundisha Kiswahili na somo la Hisabati katika Shule ya Longonot Academy, eneo la Lari, Kiambu na kuamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa masomo hayo miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya FGCK Salome Academy, Kiambu mnamo 2014 akiwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Akiwa hapo, alijulikana sana kwa msemo wake ‘Operesheni Vuka alama ya 80 katika Kiswahili.’

Kutokana na juhudi za wanafunzi wake na ushirikiano mkubwa kutoka kwa walimu wenzake idarani, somo la Kiswahili liliibuka la kwanza katika eneobunge zima la Lari katika mtihani wa KCPE 2015. Kwa kipindi cha miaka mitatu aliyohudumu shuleni Salome

Academy, Mbugua alifanikiwa sana kuwashawishi wanafunzi wake kukipenda Kiswahili na kubadili mtazamo hasi waliokuwa nao kwa lugha hiyo awali.

Kwa pamoja na walimu mbalimbali kutoka shule jirani, alianzisha mipango ya kuwashirikisha wanafunzi wake katika midahalo, warsha na makongamano. Hatua hiyo iliwapa watahiniwa wa KCPE Kiswahili jukwaa bora la kukuza vipaji vyao vya ulumbi, kunoa makali yao katika uandishi wa insha na pia kupiga msasa sarufi ambayo ni uti wa mgongo wa uandishi na uzungumzaji wa Kiswahili bora.

Isitoshe, alianzisha Jarida la Mwenge wa Kiswahili. Chapisho hilo liliwatia motisha wanafunzi na kuinua pakubwa viwango vyao vya ubunifu kiasi kuwa nyingi za insha bora walizoziandika zilichapishwa mara kwa mara katika jarida hilo.

Mnamo Agosti 2016, Mbugua alijiunga na Shule ya Msingi ya St Paul’s Kinangop ambako ushirikiano wake na Bw Gisheha na mwalimu Ndung’u ulichangia alama wastani ya 82 iliyozolewa na wanafunzi wa shule hiyo katika mtihani wa KCPE Kiswahili mnamo 2016. Atangaye sana na jua hujua. Ilikuwa hadi Januari 2017 ambapo Mbugua alijiunga na Shule ya Msingi ya Kijabe Intergity.

Hapo, alianza kuwashirikisha wanafunzi wake katika Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili la Taifa Leo. Mwanafunzi wake Nancy Muthoni aliibuka wa kwanza katika mkumbo wa Juni 2018 baada ya kuwazidi maarifa washiriki wote wengine wa shindano hilo kutoka eneo la Kati ya Kenya. Uanachama wake katika Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) umemwezesha kuhudhuria makongamano mengi ndani na nje ya Kenya. Nia yake kubwa imekuwa ni kuhakikisha kwamba beramu ya Kiswahili inazidi kupepea.

Uandishi

Mbugua anaamini kwamba safari yake ya uandishi ilianza tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili, Bi Gishina na aliyekuwa Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya Kirenga, Bw Karanja. Walimu hawa walimhimiza mno kwa kuzisoma insha zake gwarideni na pia kuziangika kwenye kuta madarasani na majilisini.

Alipojiunga na Shule ya Upili ya Nyahururu, alijiunga na Chama cha Uandishi kilichomteua kuwa Mhariri Mkuu. Wadhifa huo ulimpa msukumo wa kujitosa kabisa katika ulingo wa uandishi na akatunga mswada wa tamthilia yake ya kwanza mnamo 2012.

Baadaye mwaka huo, alitunga mswada wa kitabu ‘The Covert Mission’ kilichochapishwa kwa jina la profesa mmoja wa humu nchini! Angefanya nini ilhali kaida ya maisha siku zote huwa ni mnyonge msonge? Mnamo 2014, Mbugua alikifyatua kitabu ‘Sayari ya Insha’. Akitawaliwa na msukumo wa kuwafaa waandishi chipukizi ili nao wasionje machungu ya matapeli waliovuna na kula jasho la ukulima wake awali, Mbugua alianzisha kampuni ya uchapishaji ya Woodvillas Publishers mwishoni mwa 2015.

Mnamo 2017, alitoa kitabu ‘Adventure in the Spirit Land’ kabla ya kuchapishiwa ‘Kigoda ni Changu’ jijini Dar es Salaam, Tanzania. Kitabu hicho kilichovuma sana nchini Tanzania kilifanyiwa tahakiki na gazeti hili la Taifa Leo mnamo Agosti 1, 2018.

Mwanzoni mwa mwaka wa 2018, Mbugua alichapisha kitabu ‘Yohana Mtundu Afunzwa Adabu’ ambacho kwa maoni yake, kitawafaa sana watoto waliopo chini ya mtaala mpya wa 2-6-6-3. Kwa sasa anahitimisha maandalizi ya riwaya ‘The Chain of Tragedies’ itakayochapishwa wakati wowote.

Jivunio

Huwezi kujua kazi aliyofanya mkulima hadi atakapovuna mavuno mazuri. Mbugua anamstahi sana mkewe Monicah pamoja na watoto Shantel na Shantel.

Anawaonea fahari wengi wa wanafunzi wake ambao wamezifuata nyayo zake na kuwa walimu wa Kiswahili. Anajivunia pia kuwa kiini cha hamasa ambayo kwa sasa inawavaa Bw Kigo na Bi Carol Kamau katika ulingo wa utunzi wa kazi za kibunifu.