GWIJI WA WIKI: Robert ‘Ramtez’ Elijah

GWIJI WA WIKI: Robert ‘Ramtez’ Elijah

Na CHRIS ADUNGO

PANIA kuwa mfano wa kuigwa na wenzako ili hatimaye uache jina zuri duniani.

Lenga kuwa sehemu ya mabingwa watakaotajwa kwa wema waliotenda na ubora wa kazi walizofanya kabla ya kufunga safari isiyo na marejeo.

Jifunze kutokata tamaa, dumisha nidhamu, shindana na wakati, kuwa mtu mwenye msimamo na ujiamini katika kila hali. Jitume katika kazi yako, kuwa na moyo wa kushirikiana na watu wengine na umtumainie Mungu siku zote.

Huu ni ushairi wa Robert ‘Ramtez’ Elijah – mwanahabari chipukizi, mwigizaji, mjasiriamali na mfawidhi wa sherehe ambaye ni mpenzi kindakindaki wa Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Ramtez alizaliwa katika eneo la Mbitini, Kaunti ya Kitui. Ndiye mwana wa pili katika familia ya watoto watatu wa Bi Ruth Robert na marehemu Bw Robert Musee. Nduguze ni Geoffrey na Caleb.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya New Hope Mbitini. Baadaye alijiunga na Shule ya Msingi ya St Stephen’s Kaveta, Kitui alikosomea kati ya 2009 na 2013.

Ramtez alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya St Thomas Aquinas Kalawa Boys, Kitui (2014-2017).

Kwa sasa yeye ni mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika taaluma ya Habari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Egerton (Bewa la Nakuru Mjini). Anatazamia kuhitimu mwaka huu.

Aliyemwamshia ari ya kuchapukia Kiswahili ni mwalimu Nyamai aliyemfundisha katika shule ya upili. “Alinipokeza malezi bora ya kiakademia na akapalilia vizuri mche wa Kiswahili ambao kwa sasa ni mti maridadi,” anasema.

Vipaji vya uigizaji, kucheza vyombo vya muziki na utunzi wa mashairi vilianza kujikuza na kudhihirika ndani ya Ramtez katika shule ya msingi.

Akiwa mwanafunzi wa Darasa la Sita, alimtungia aliyekuwa Waziri wa Maji, Mhe Bi Charity Ngilu, shairi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na akatuzwa Sh5,000. Bi Ngilu kwa sasa ni Gavana wa Kaunti ya Kitui.

Ramtez aliwahi kuongoza makundi mbalimbali ya wanafunzi kutoka Kalawa Boys kuwakilisha shule hiyo katika tamasha za kitaifa za muziki na drama na wakajizolea tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha.

Anatambua pia upekee wa mchango wa Bw Matata anayezidi kumshika mkono kadri anavyojitahidi kupanda vidato vya mafanikio katika safari ya maisha. Bw Matata kwa sasa ndiye msimamizi mkuu wa masuala ya utamaduni na burudani katika Chuo Kikuu cha Egerton.

“Hajawahi kuchoka wala haelekei kufanya hivyo. Matarajio yake ni makubwa na matamanio yake ni kuniona nikiendelea kupanua wigo wa burudani na kuwanda katika ulingo wa sanaa na uanahabari.”

“Mwingine anayenishajiisha maishani ni mama mzazi ambaye alinilea kwa misingi ya kumcha Mungu na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo.”

Ramtez anahisi kwamba fahari zaidi hii leo ingalikuwa kwa baba mzazi kumsikiliza redioni akitema maneno anayoyaita kwa Kiswahili – ajivunie tija, aone fahari na kupata kitulizo kamili cha nafsi kwa kumsherehekea mwanawe.

MCHANGO KITAALUMA

Hata kabla ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu, Ramtez tayari ameanza kujihusisha na taaluma yake. Tangu Oktoba 2020, amekuwa mwanahabari wa Egerton Radio 101.7 FM.

Mbali na kutangaza taarifa, yeye hueendesha kipindi ‘Link-Up Sato’ ambacho hupeperushwa hewani kila Jumamosi. Aliwahi kuhudumu katika idhaa ya Hero Radio 99.0 FM kati ya Disemba 2019 na Machi 2020 akishiriki uendeshaji wa kipindi ‘My Generation My Assignment’.

Kwa kutumia utajiri wa kipaji chake cha ulumbi, Ramtez amepiga hatua kubwa katika juhudi za kuwekea taaluma ya uanahabari uhai. Anapania siku zote kuoanisha talanta na taaluma anayoisomea.

Upekee huo umemvunia fursa nyingi za kuwa mfawidhi wa sherehe pamoja na kutia sauti matangazo ya biashara kutoka kampuni au mashirika mbalimbali.

Ramtez amefanya na anazidi kufanya mambo makuu katika ulingo wa Kiswahili. Zaidi ya kushiriki michezo ya kuigiza, yeye hutunga mashairi kwa ajili mashindano ya viwango mbalimbali katika tamasha za muziki na drama.

CHANJA KIJANJA

Zaidi ya kuwa mfawidhi wa shehere kwa malipo au kwa kujitolea, Ramtez pia huendesha masimulizi kuhusu visa vya wasanii – machale na wanamuziki kutoka Afrika Mashariki – kwenye YouTube (Chanja Kijanja).

Jukwaa hili huwapa mashabiki fursa maridhawa ya kuwafahamu wasanii wao kwa kina – kitaaluma na katika maisha ya kawaida.

Anapojitahidi kuiwekea dira taaluma yake, Ramtez pia amejifunga kibwebwe kuhakikisha kuwa anatamba katika ulingo wa burudani kwa lengo la kuridhisha nafsi na kuwapa mashabiki wake ‘kitu’ cha kujivunia.

Anaishi kwa imani kwamba mvuto na mguso kwenye mrindimo wa sauti yake utakuja kuwa kitambulisho chake katika majukwaa ya burudani, uanahabari na matangazo ya biashara.

Ramtez ni mwanablogu anayeshiriki mijadala mingi ya kitaaluma kupitia vipindi vya redio, runinga na kumbi za Kiswahili mitandaoni. Amezamia pia uuzaji wa sharubati; kazi ambayo humpa tonge la kila siku.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kufikia viwango vya Omary Tambwe Lil Ommy (Wasafi), Mzazi Willy M. Tuva (Citizen) na Chris Da Bass (Milele FM).

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Mashekhe wanachangia kudorora kwa...

Uingereza pazuri kutinga fainali ya Euro baada ya kudengua...