Makala

GWIJI WA WIKI: Samuel Mwenda

September 4th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUWA na kipaji ni kama kuwa na gari ambalo limejaa petroli.

Petroli ni mojawapo ya vitu vinavyohitajika ili gari liweze kufanya kazi. Iwapo sehemu nyinginezo hazifanyi kazi, gari litakwama.

Kwa hivyo, mtu huhitaji zaidi ya kipaji. Bidii humwezesha mwanadamu kutambua na kuzindua kipawa chake. Ustahimilivu na nidhamu huwasha azma ya moto usiozima wa maendeleo.

Kumcha Mungu humpa mtu mwelekeo ili ajue umuhimu wake wa kuishi duniani na kumwezesha kunufaika kutokana na mazingira yake.

Pia humfanya kufahamu umuhimu wa watu wengine katika maisha yake. Yampasa mtu kuelewa anakotoka na kuwa na taswira ya anakoenda.

Anapolenga kufanya jambo, asipoteze mtazamo wake wala kuyumbishwa na sauti zinazomhimiza kukata tamaa. Iwapo atajikwaa, kuteleza au kuanguka, ajitahidi kujizoa na kuendelea na safari.

Mazoezi ya kila mara huimarisha tajriba.

Tajriba hupatikana kwa kujifunza kutoka kwa wale waliokutangulia na kujaribisha kila mbinu uliyojifunza. Kwa kufanya hivyo, itakuwa rahisi kufahamu mbinu inayokufaa kujipiga msasa.

Mtu asiwadharau watu anaowafanyia kazi hata wawe wadogo au maskini. Huenda atahitaji msaada wao baadaye. Heshima na unyenyekevu huvutia baraka. Mtu anapaswa kufanya kazi bila kushurutishwa na wakubwa wake.

Jambo hili litaimarisha uwezo wake wa kuongoza na pia kumpa ujuzi wa kuanzisha na kusimamia kazi zake binafsi.

Huu ndio ushauri wa Bw Samuel Mwenda, mwalimu mwenye uzoefu wa miaka mingi katika ufundishaji wa Kiswahili, malenga stadi, mwandishi shupavu, mwimbaji na mwanakwaya maarufu.

MAISHA YA AWALI

Mwenda alizaliwa mnamo 1970 katika kijiji cha Tutua, eneo la Buuri, Kaunti ya Meru akiwa mwanambee wa Bi Monica Ntibuka na Bw Daniel M’Mutungi.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Tutua hadi mwishoni mwa 1982 alipohamia Shule ya Msingi ya Kithuene.

Alifanya mtihani wa KCPE mnamo 1987 na kupata nafasi katika Shule ya Upili ya Gikumene katika Kaunti ya Meru mnamo 1988. Aliufanya mtihani wake wa KCSE shuleni humo mwishoni mwa 1991. Alilelewa na nyanya yake hayati Tabitha Nyoroka Bagine ambaye alikuwa mwalimu wake wa kwanza.

Hadithi nzuri alizomsimulia zilimjengea msingi imara wa kuwa mwalimu na mwandishi mahiri.

USOMI

Mnamo 1995, Mwenda alijiunga na Chuo cha Walimu cha Migori kusomea Cheti cha Ualimu (P1). Alifuzu Julai 1997.

Akiwa huko, alikutana na walimu wa Kiswahili Bw Muhere na Bw J. Oyucho ambao walimhimiza kuendelea na elimu ya juu ili kuendeleza ujuzi wake wa Kiswahili. Hamu ya kujiendeleza kitaaluma ilimfanya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 2003 kusomea Shahada ya Ualimu (Kiswahili na Fasihi ya Kiingereza). Alifuzu mwishoni mwa 2008.

Katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alitangamana na kusoma kazi za wahadhiri wengi wa Kiswahili na Fasihi ya

Kiingereza ambao walichochea sana hamu yake ya uandishi. Wahadhiri hawa ni pamoja na: Prof Mwenda Mbatiah, Prof Rayya Timammy, Prof Iribe Mwangi, Prof Guantai Mboroki, Dkt Hezron Mogambi, Dkt Kimingichi Wabende, Prof Catherine Ndungo, Dkt Evans Mbuthia na Dkt Judith Jefwa.

Pia alikutana na mwandishi na mwanafunzi mwenzake, Bw Mutahi Miricho. Mnamo 2009, Mwenda alijiunga na Chuo Kikuu cha Chuka kusomea Shahada ya Uzamili katika Kiswahili.

Alifuzu mwishoni mwa mwaka wa 2015 baada ya kuandika tasnifu yake “Athari za jinsia katika mielekeo ya kupendelewa kwa Kiswahili na umuhimu wake katika matokeo ya mtihani: Tathmini ya shule za upili wilaya ya Igembe Kaskazini, Kaunti ya Meru –Kenya”. Kazi hii ilisimamiwa na Prof Mwenda Mukuthuria na Bw Enock Matundura. Katika Chuo Kikuu cha Chuka, Mwenda alitangamana na wahadhiri walioendelea kuwasha moto wa uandishi ndani yake.

Pamoja na Prof Mukuthuria na Bw Matundura, mawaidha ya Prof John Kobia, Dkt Kinoti M’Ngaruthi, Dkt Allan Mugambi, Dkt John Kamoyo yalimfaa sana katika safari ya uandishi. Somo la uandishi wa kubuni walilofundishwa na Bw Matundura lilimfanya kujitosa kabisa katika uandishi wa kazi za bunilizi.