GWIJI WA WIKI: Sharon Nafula Wekesa

GWIJI WA WIKI: Sharon Nafula Wekesa

Na CHRIS ADUNGO

MAFANIKIO ya mtu hayapimwi kwa utajiri wa mali na wingi wa fedha, bali kwa ukubwa wa alama zenye kumbukumbu nzuri anazoziacha katika nyoyo na nafsi za wengine.

Tupo jinsi tulivyo kwa sababu ubora tulio nao umechangiwa na watu wengine. Tazama nyuma uone mchango wa watu hao kisha uwapongeze.

Hakuna aliye na uwezo wa kuzima ndoto zako za maisha isipokuwa wewe mwenyewe. Changamkia fursa adimu utakazozipata za kukupigisha hatua kitaaluma. Jiamini na ufanye hivyo kwa kani na idili.

Huu ndio ushauri wa Bi Sharon Nafula Wekesa – mwandishi chipukizi na mlezi wa vipaji ambaye sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Nakuru Whizzkids.

MAISHA YA AWALI: Sharon alizaliwa Novemba 1994 katika kijiji cha Wehoya, viungani mwa mji wa Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia.

Ndiye mtoto wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bi Margaret – mke wa kwanza wa Bw Peter Wekesa ambaye mkewe wa pili, Bi Veronica, amejaliwa watoto watano.

Sharon alilelewa eneo la Moi Farm Kitale katika utamaduni uliosisitiza ulazima wa mtoto kuadhibiwa na kushauriwa na mzazi yeyote kwa kuwa jukumu la ulezi lilikuwa la jamii nzima. Wavyele wake pia walimrudi kila alipokosea. Hilo lilimfanya kukua akiwa mtoto muadilifu na mwenye bidii.

Hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ni ndoto iliyoanza kujikuza ndani ya Sharon tangu utotoni. Mara si haba, alijipata akiiga sauti za wanahabari maarufu na akapendwa na watu kutokana na ‘sauti yake ya utangazaji’.

Nyanya yake, Leonida Nafula, alikuwa mwepesi wa kumpagaza majina ya watangazaji mashuhuri bila kufahamu kwamba alikuwa akipanda mbegu ya uanahabari iliyoota na kuwa mche maridadi ambao sasa unasubiri kuchanua ndani ya nafsi ya mjukuu wake huyu.

Sharon alisomea katika Shule ya Msingi ya Simatwet hadi darasa la saba kabla ya kuhamia katika Shule ya Msingi ya Mosoriot.

Alikuwa na mazoea ya kuwahi nyumbani kila siku saa saba mchana. Hakufanya hivyo kwa ajili ya chakula cha mchana tu. Maazimio yake makuu yalikuwa kupata fursa adhimu za kusikiliza taarifa za habari zikisomwa na watangazaji aliowastahi na kushabikia.

Japo alifaulu vyema katika mtihani wa KCPE na kuitwa kujiunga na mojawapo ya sekondari za haiba, uchechefu wa karo ulimfanya arudishwe Wehoya kusomea katika shule ya kutwa ya Friends Sirende.

Akiwa huko, alilelewa na ami yake, Andrew Wabwile pamoja na mkewe Everlyne. Sharon aliwaaga nduguze na kuanza ukurasa mpya wa maisha pamoja na binamu zake Florian, Fortune, Fenil na Fidel.

Licha ya changamoto za kila sampuli alizokumbana nazo, alizidi kuuma uzi masomoni. Alibahatika kujiunga na Chama cha Uanahabari shuleni na akapalilia kipaji chake cha utangazaji na utunzi wa kazi bunilizi.

Alifanya mtihani wa KCSE katika mwaka wa 2014 na akajiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Nakuru mnamo Februari 2016.

Akiwa mgeni wa wiki mbili pekee chuoni humo, alipata fursa ya kushiriki kipindi cha makuzi ya Kiswahili katika runinga ya KTN News. Huo ulikuwa mwanzo wake wa kuwa mwendeshaji wa mijadala ya kitaaluma kupitia vipindi vya lugha redioni, runingani na mitandaoni.

MCHANGO KITAALUMA: Baada ya kuhitimu elimu ya chuoni, Sharon alikuwa mtangazaji na ripota wa kujitolea katika stesheni ya Mitume Radio mjini Kitale. Alihudumu huko kwa kipindi cha miezi sita. Akiwa mwanafunzi, alikuwa na mazoea ya kukitembelea kituo hicho mara kwa mara nyakati za likizo na akajifunza mengi katika tasnia ya uanahabari.

Ilikuwa hadi 2018 ambapo alirejea Nakuru kusaka ajira ya ualimu. Maamuzi ya kujitosa katika ulingo wa kiakademia na hata kusomea ualimu ni zao la kuhimizwa na Bi Josephine Onyango aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya upili.

Zaidi ya kumpa kazi ya kuchambua vitabu vya fasihi darasani, Bi Onyango alimteua Sharon mara kwa mara kusoma vifungu vya somo la Ufahamu na kumpa nafasi maridhawa za kuhutubu gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Wazazi nao walimnunulia vitabu vingi vya hadithi. Alipata majukwaa maridhawa ya kunoa kipaji chake cha ulumbi, kuinua kiwango cha umilisi wa lugha na kukichapukia Kiswahili kwa utashi.

UANDISHI: Mapenzi ya kusoma magazeti na vitabu vya hadithi yalimwamshia Sharon hamu ya kuandika kazi bunilizi kila alipokuwa hana shughuli maalumu za kufanya.

Ingawa angezichana tena kurasa alizoandika kwa hofu kwamba alichokisarifu hakikuwa chochote wala lolote, walimu waliotambua utajiri wa kipaji chake walimhimiza apige mbizi katika bahari pana ya utunzi.

Nyingi za insha alizozitunga zilimzolea tuzo za kutamanisha kutoka kwa walimu wake. Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali na hata kuchapishwa katika gazeti hili. Uandishi wa Sharon umeathiriwa pakubwa na kazi za marehemu Profesa Ken Walibora.

Kufikia sasa, amechapishiwa hadithi fupi kadhaa katika antholojia mbalimbali kama vile ‘Maisha Karakana na Hadithi Nyingine’, ‘Harufu ya Jehanamu na Hadithi Nyingine’ na Mateka na Hadithi Nyingine’. Amechangia pia mashairi katika diwani za ‘Wosia Na Mashairi Mengine’ na ‘Malenga wa Kenya’ na ‘Tasnia ya Ushairi’.

JIVUNIO: Ndoto ya Sharon ni kufikia upeo wa taaluma yake, kuwa mwandishi tajika na mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Anatambua upekee wa mchango wa Bw Timothy Omusikoyo Sumba anayezidi kumshika mkono kadri anavyojitahidi kupanda vidato vya mafanikio katika safari ya uandishi.

“Hajawahi kuchoka wala haelekei kufanya hivyo. Matarajio yake ni makubwa na matamanio yake ni kuniona nikiendelea kupanua wigo na kuwanda katika ulingo wa sanaa.”

Anamstahi sana ami yake Andrew na mkewe Everlyne ambao walimtwaa udogoni, kumchukua kama mwana wao na kumgharimia masomo yake ya sekondari.

“Mbali na kunishajiisha maishani, walinilea kwa misingi ya kumcha Mungu na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo,” anasema.

You can share this post!

Mawakili waliowakilisha Jumwa walia kuitiwa DCI

Maji ya mafuriko Mto Ngong yatatiza usafiri kati ya mitaa...