Makala

GWIJI WA WIKI: Silvester Makau

October 16th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

SAWA na bidhaa yoyote nyingine, Kiswahili kina uwezo wa kuuzwa na kununuliwa. Kiswahili kinaweza kukutoa hapa na kukuweka hapo kabla ya kukufikisha pale.

Kuna idadi kubwa ya watu ambao kwa sasa wanajivunia mafao ya Kiswahili ulimwenguni. Siri ya mafanikio yao imekuwa ni kufuata misukumo ya ndani ya nafsi zao hadi ndoto zao zikatimia.

Kwa hivyo, lenga kuwa bora katika chochote unachoteua kukishughulikia. Kwa kuwa Mola ndiye mwelekezi wa hatua zote tunazozipiga maishani, inatulazimu kumweka mbele siku zote. Kufaulu katika jambo lolote kunahitaji mtu kuwa na maono na kutenda mema bila ya kudhamiria malipo. Nidhamu, bidii na imani ni kati ya mambo mengine yanayochangia mafanikio ya binadamu.

Huu ndio ushauri wa Bw Silvester Lunyiro Makau – mshairi shupavu, mwanadensi stadi na mwandishi chipukizi ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo cha Walimu cha Eregi, Kaunti ua Kakamega.

Maisha ya awali

Makau alizaliwa mnamo Juni 30, 1978 katika kijiji cha Matawa, eneo la Mumias Magharibi, Kaunti ya Kakamega. Ni kitinda mimba katika familia ya watoto sita wa Mama Josphine Chibete na marehemu Bw Joseph Makau Wayugu aliyekuwa mwalimu na askari wa magereza. Makau ana mke Arnolda Lunyiro Wangatia ambaye kwa sasa ni mwalimu wa somo la Sayansi, Kiswahili na Hisabati katika Shule ya Msingi ya Nambale Urban, Kaunti ya Busia. Mungu amewajalia watoto watatu: Emmanuel, Faith na Joseph Louise.

Elimu

Makau alianza safari yake ya masomo katika chekechea ya Matawa mnamo 1986 chini ya mwalimu Adhiambo. Alijiunga baadaye na Shule ya Msingi ya Matawa hadi mwaka wa 1994. Akiwa huko, alikuwa mwanariadha hodari na mwanakundi wa 4K-Club.

Ndoto ya kuimarika kwake kilugha ilitiwa mshawasha na waliokuwa walimu wake Bw Zaddock Ingutia (Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya Matungu), Tom Ambani (mwalimu katika Shule ya Upili ya Mumias Muslim, mchoraji hodari na msanii maarufu), Moses Karakacha (mwalimu katika Shule ya Msingi ya Ichinga) na Mwinamo Akunda ambaye hadi kustaafu kwake, alikuwa Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya Matawa.

Hawa ni baadhi ya walimu waliompokeza malezi bora zaidi ya kiakademia na kumwamshia ari ya kukipigia chapuo Kiswahili baada ya kumshirikisha katika mashindano mbalimbali ya kusoma ufahamu kwa ufasaha.

Makau aliibuka mshindi wa mapambano hayo katika shule nzima tangu akiwa mwanafunzi wa darasa la sita na kujizolea zawadi tele za haiba zilizompandisha katika majukwaa ya kutukuzwa kwa Kiswahili.

Mnamo 1995 alijiunga na Shule ya Kiseminari katika eneo la Mukumu, Kaunti ya Kakamega kwa minajili ya masomo ya sekondari.

Askofu Maurice Muhatia ambaye kwa sasa anahudumu katika Kaunti ya Nakuru alichangia pakubwa kuinua umilisi wa Makau katika Kiswahili baada ya kumtanguliza vyema katika usomaji wa riwaya ‘Shamba la Wanyama’.

Ukakamavu wa Makau ulimfanya kulipenda somo la Kiswahili; na hasa uandishi wa Insha.

Mnamo 1998 alihamia hadi Seminari ya Mama wa Mitume (Mother of Apostles Seminary) mjini Eldoret ambapo alikutana na mwalimu wa Kiswahili Bw Musumba aliyemtandikia zulia zuri la kukichangamkia Kiswahili.

Baada ya kukamilisha mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 1998, Makau alianza kufundisha katika Shule ya Msingi ya Matawa.

Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Mumias D.E.B. Katika shule hizi, alifundisha Kiswahili na masomo ya Sayansi, Zaraa na Biashara. Wengi wa wanafunzi wake walipasi mitihani yao kwa alama za juu.

Mnamo 2001, Makau alijiunga na Chuo cha Walimu cha Eregi na akawa kiongozi wa Y.C.S na mchezaji mashuhuri wa ngoma ya Isukuti hadi kiwango cha kitaifa. Anamkumbuka mwalimu wake wa Kiswahili Bw Fredrick Oduori Wafula aliyemtia hamasa ya kukipenda Kiswahili na kumpa mbinu na mikakati ya kulifunza somo lenyewe kwa ustadi zaidi hatimaye akawa mwalimu bora.

Pia anatambua ukubwa wa mchango wa mwalimu Kizito Mugali, mnenaji mahiri wa Kiswahili ambaye kwa sasa ni mbunge wa Shinyalu, Kakamega. Ni Bw Mugali ndiye aliyemsadikisha Makau kwamba Kiswahili ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ajira na uvumbuzi.

Baada ya kuhitimu kuwa mwalimu wa kiwango cha P1 mnamo 2002, Makau alianza kufundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Mumias Central kabla ya kuhamia Mumias Township kisha Imakale katika eneo la Matungu.

Aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) mnamo 2004 na kutumwa katika Shule ya Msingi ya Mwitoti, Mumias alikohudumu hadi 2007.

Alifundisha Mumias D.E.B kati ya 2008 na 2011 kisha kuhamishiwa katika Shule ya Msingi ya Lureko, Mumias alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake. Alifundisha huko hadi 2014.

Usomi

Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimchochea Makau kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 2007 kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini). Alifuzu mwishoni mwa 2011. Ari ya kukichapukia Kiswahili akiwa chuoni ni zao la kutangamana kwa karibu na wahadhiri wake Prof Rayya Timammy, Dkt Evans Mbuthia, Prof Iribe Mwangi, Dkt Mugambi, Dkt Ayub Mukhwana na Prof Kithaka Wa Mberia.

Mnamo 2014, Makau alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya uzamili katika Kiswahili.

Kati ya mikota wa lugha waliomlea zaidi kitaaluma akiwa huko ni Dkt Wafula, Dkt Pamela Ngugi, Dkt Mwihaki, Dkt Arege, Dkt Onyango, Dkt Chacha, Dkt Wanjala, Dkt Osore na Prof Catherine Ndungo.

Anatazamia kufuzu mwakani baada ya kuwasilisha tasnifu “Uwiano wa Picha na Matini katika Fasihi ya Watoto kwa kurejelea riwaya teule ‘Kesho! Kesho!’ na ‘Werevu wa Juma’ chini ya usimamizi na uelekezi wa Dkt Ngugi na Prof Ndungo.

Kuanzia mwaka wa 2016, Makau amekuwa mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo cha Walimu cha Eregi. Anawashukuru Bw Mokono (mwalimu wa Kiswahili), Bw Wafula Oduori (Mtahihi Mkuu wa Baraza la Mitihani la Kenya) na Bw Mirikau Suleiman (mwandishi wa vitabu vya vyuo vya walimu) kwa uelekezi wao wa mara kwa mara unaozidi kuchangia matokeo bora ya wanafunzi wake katika mitihani ya kitaifa ya PTE.

Uandishi

Makau ameandika na kuchapishiwa makala mbalimbali ya kitaaluma. Miongoni mwa kazi zake ni ‘Lugha na Mtoto’, ‘Lugha ya Pili’, ‘Mfumo wa 8-4-4’, Mtaala wa Umilisi (CBC)’, ‘Nafasi ya Kiswahili katika Ukadiriaji wa Mtaala wa Umilisi Gredi ya 3’, ‘Jinsi Mtaala wa Umilisi (CBC) Hujenga Stadi za Kiswahili’, ‘Ni Mtihani ama ni Mkadiriaji wa Mtaala wa Umilisi (CBC)?’ na ‘Ufunzaji wa Sauti ‘t’ na ‘d’ kwa Kutumia Mtindo wa Tusome na CBC’.

Kwa sasa anaandaa kitabu cha hadithi kwa wanafunzi wa kiwango cha Gredi ya 2 kiitwacho ‘Njiwa’. Mnamo 2019, Makau alitunga shairi ‘IOM Japan Hoyee!’ lililokaririwa na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Kwale Girls chini ya uelekezi wa mwalimu wao Bi Zainab Ramadhan kwa nia ya kuwashukuru wafadhili wa shule hiyo.

Jivunio

Makau anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Baadhi yao ni Anne Waswa ambaye ni mhadhiri wa Kemia nchini Amerika, Dkt Rebecca Wanga, mwalimu Bonface Otuko wa Shule ya Upili ya Matawa, mwalimu Magaret Auma Were wa Shule ya Sekondari ya Lufumbo, mwalimu Martha wa Kaunti ya Nyeri na mwalimu Isabella Wangatia wa Shule ya Upili ya Khayo, Kaunti ya Busia.

Anamstahi pakubwa Bi Alice Ghettu, mwalimu wa Kiswahili na somo la Sayansi Kimu ambaye amesimama naye kwa hali na mali ili kufanikisha kila hatua anayoipiga kitaaluma.

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto zake za kuwa profesa wa Kiswahili, mwandishi maarufu, mhariri stadi na mwanadiplomasia mashuhuri, Makau anajivunia kuwa kiini cha motisha na hamasa ambayo kwa sasa inawatawala walimu wengi anaoshirikiana nao katika jitihada za kukitetea Kiswahili.