Makala

GWIJI WA WIKI: Timothy Kinoti M’Ngaruthi

March 29th, 2018 4 min read

BIDII na maombi huandamana kwani imani bila matendo imekufa! Huu ndio ushauri wa Dkt
Timothy Kinoti M’Ngaruthi – mwandishi, mtafiti, mhariri na mhadhiri wa Kiswahili.

MAISHA YA AWALI
Dkt Kinoti alizaliwa kijijini Kanthungu, kata ya Ruiri, katika Kaunti ya Meru mnamo 1967 akiwa kitindamimba katika familia ya watoto tisa. Alisomea katika Shule ya Msingi ya Loire (1975-1983), Shule ya Upili ya Chuka (1984-1987) na Shule ya Upili ya Kanyakine (1988-1989).

Ana Shahada ya Elimu (Kiswahili na Jiografia) kutoka Chuo Kikuu cha Egerton (1990-1994), Uzamili katika Kiswahili (Chuo Kikuu cha Kenyatta, 2008) na Uzamifu katika Kiswahili (Chuo Kikuu cha Chuka, 2015).

 

HUJAFA HUJAUMBIKA
Dkt Kinoti hakufanya vyema katika mtihani wa Darasa la Saba wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Shule ya Msingi (CPE) mnamo 1982 kwani aliambulia jumla ya alama 21 kwa 36. Baada ya kukosa nafasi ya kuendelea na masomo ya shule ya upili, aliamua kujiunga na chuo cha ufundi kujifunza uashi.

Siku chache kabla ya kujiunga na Isiolo Village Polytechnic, aliyekuwa mwalimu wake wa shule ya msingi, Bw Justus Murira aliwasili nyumbani kwao na kumshawishi kurudia Darasa la Saba.

Aliporejea shuleni shingo upande, hakujua kwamba katika mtihani wa CPE wa 1983, angeibuka kuwa mwanafunzi wa pili bora katika shule yao kwa kuzoa jumla ya alama 28! Lakini furaha yake iliyeyuka ghafla baada ya kukosa karo ya kujiunga na Shule ya Upili ya Chuka kwani mnamo 1984, kulitokea baa la njaa nchini Kenya linalokumbukwa hadi leo kutokana na kuwasili kwa msaada wa mahindi ya manjano kutoka Marekani.

Iliwabidi wazazi wake Kinoti – mzee M’Ngaruthi M’Kirigia na mama Grace Kaguri, kuuza kipande cha ardhi walichokuwa wakikitegemea sana kwa chakula katika kata ya Kambakia.

Alipojiunga na Kidato cha Kwanza, alikuwa tayari amepitwa na mengi kwani ilichukuwa muda mrefu kupata mnunuzi wa ardhi yao. Ingawa alipitia changamoto tele, bidii za wazazi wake zilizoandamana na maombi zilimwezesha kupata jumla ya alama 20 katika Kiwango cha Kwanza (Division One) katika mtihani wa Kidato cha Nne (KCE) wa 1987.

Alipojiunga na Shule ya Upili ya Kanyakine, alifanya vyema katika mtihani wa Kidato cha Sita (KACE) mnamo 1989 kwa kuzoa jumla ya alama 13 kwa 18.

Vitabu alivyochapisha hadi sasa ni Fasihi Simulizi na Utamaduni (Jomo Kenyatta Foundation, 2008) kinachotumiwa na wanafunzi na walimu katika shule za upili na vyuo vikuu nchini na ughaibuni, na Miale ya Mashariki:Mashairi na Mwongozo wa Uchambuzi (Nsemia Inc. Ontario, 2012). Picha/ Chris Adungo

UALIMU
Dkt Kinoti amewahi kufunza katika Shule ya Upili ya Mataara, Thika (1994-1996), Shule ya Wasichana ya Kanjalu, Meru (1996-1999) na shule ya Wasichana ya Ruiri, Meru (2000-2010). Kwa miaka kadha, alikuwa mtahini wa kitaifa wa Karatasi yaTatu ya KCSE (Fasihi ya Kiswahili).

Aidha, alikuwa akitunga mashairi na kuwaandaa wanafunzi kwa mashindano ya kitaifa ya muziki na drama, mbali na kuwa mkaguzi katika tamasha mbalimbali, yakiwemo mashindano ya muziki na ushairi makanisani.

Amewahi kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kimethodisti (KeMU) ambamo alikuwa Mkuu wa Idara ya Elimu (2015-2016) kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Embu mnamo Septemba 2016 na kuteuliwa katika kamati mbalimbali za chuo.

Hizi ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha za Kitamaduni, Kamati ya Uhariri wa Miswada ya Sera za Chuo Kikuu, Mhariri wa Jarida la Flashlight na Mlezi wa Chama cha Kiswahili, miongoni mwa majukumu mengine.

Isitoshe, amewahi kufunza kozi kadha za Uzamili katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya na Chuo Kikuu cha Chuka akiwa mhadhiri wa muda.

 

UANDISHI
Aligundua kipawa chake cha uandishi alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Insha alizoziandika kwa Kiingereza zilisifika sana shuleni kote na pia kuongoza katika mitihani ya mwigo tarafani. Wakati huo, somo la Kiswahili halikutiliwa maanani katika shule za msingi kwani halikuwa likitahiniwa mwishoni mwa Darasa la Saba.

Hata hivyo, palikuwepo walimu wawili – Bi Jacinta Muthamia na Bw Rwigi, ambao walijitolea kuwafunza Kiswahili wakati walimu wengine walipokosa kuona maana ya somo hilo.

Juhudi za walimu hao pamoja na zile za babaye mzazi ambaye alimfunza kuhesabu kwa Kiswahili zilimfanya Kinoti kuvutiwa na somo hilo. Pia alipenda kusikiliza mashairi yaliyoghaniwa redioni na mzee Abdalla Mwasimba.

Mwalimu wake wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Chuka, Bw Kaimenyi Marete ndiye aliyemsaidia kutambua kipawa chake hasa alipompa nafasi ya kushiriki katika kipindi cha

Sanaa ya Kiswahili kilichopeperushwa na runinga ya VoK (sasa KBC) mnamo 1987. Dkt Kinoti alishiriki mjadala ‘Kiswahili ni Lugha ya Kibantu’ na kutambuliwa na waamuzi James Kanuri na Bakari Mwarandani kuwa mwanafunzi bora zaidi miongoni mwa waliokuwa washiriki. Kipindi hicho kilimpa umaarufu mkubwa katika shule hiyo ambayo ilikuwa na zaidi ya wanafunzi 800.

Katika Shule ya Upili ya Kanyakine, alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kiswahili na Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari. Isitoshe, yeye na mwanafunzi mwenzake, Kamau Munyua (mtangazaji maarufu wa Redio Citizen) walitambuliwa kuwa waandishi rasmi wa habari na kutengewa viti maalum ndani ya basi wakati timu za shule ziliposafiri kwa mashindano ya muziki, drama na michezo.

Dkt Kinoti alipata fursa ya kipekee ya kuwa mwanahabari katika ukumbi wa KICC wakati wa Tamasha za Kitaifa za Muziki mwaka wa 1989! Walimu wake – Bi Ngaku, Bw Murugu na Bw Nkanata pia walikipalilia kipawa chake cha uandishi kwa kumuomba kutunga mashairi yaliyowasilishwa na wanafunzi wenzake katika tamasha za muziki na kupata tuzo mbalimbali.

Aidha, alishiriki katika vitengo vya nyimbo za kitamaduni na mazungumzo pamoja na kukariri na kughani mashairi aliyotunga.

Kutangamana kwake na wasomi maarufu wakiwemo Chacha Nyaigotti Chacha, Abdulaziz Lodhi, Kimani Njogu, Rocha Chimerah, Ken Walibora, John Habwe, Rayya Timammy, Catherine Ndungo, Clara Momanyi, Richard Wafula, Mwenda Mukuthuria, John Kobia na Bitugi Matundura kumemchochea kujiendeleza zaidi katika utafiti na uandishi akilenga kufikia ngazi ya uprofesa.

Vitabu alivyochapisha hadi sasa ni Fasihi Simulizi na Utamaduni (Jomo Kenyatta Foundation, 2008) kinachotumiwa na wanafunzi na walimu katika shule za upili na vyuo vikuu nchini na ughaibuni, na Miale ya Mashariki:Mashairi na Mwongozo wa Uchambuzi (Nsemia Inc. Ontario, 2012).

Diwani hii yenye mashairi 82 imeidhinishwa na KICD kutumika katika shule za upili nchini Kenya.

Pia amechapisha makala ya kitaaluma katika majarida ya kimataifa na kushiriki makongamano ya kimataifa yaliyoandaliwa na Baraza la Wanataaluma wa Kiswahili (BAWAKI), Taasisi ya Utafiti na Masomo ya Kiswahili Afrika Mashariki (RISSEA), Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Kongamano la Kwanza la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Zanzibar.

 

JIVUNIO
Dkt Kinoti ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shule ya Upili ya Rwarera na Mlezi wa Shule ya Msingi ya Kanthungu. Pia huhubiri neno la Mungu na kutoa ushauri katika makanisa na taasisi mbalimbali, mbali na kuwa mfawidhi (MC) katika sherehe mbalimbali. Katika shughuli zote, mke wake – Bi Hellen Kinoti pamoja na mabinti zake – Karwitha, Kajuju, Joy na Rehema wamekuwa nguzo kuu.