Makala

GWIJI WA WIKI: Yusuf Wambugu

May 27th, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

UKITAKA kumuua nyani, usimtazame usoni!

Kila jambo huhitaji utaratibu wa kulitekeleza.

Wazia athari za lolote utendalo, fanya mambo kwa mpangilio na uliza wajuao kwani hakuna bingwa wa mabingwa!

Usipapie kufanya jambo kwani mkamia maji hayanywi na akiyanywa humsakama. Fanya kila kitu kwa wakati wake na kwa jinsi inavyofaa. Bidii na stahamala ni sifa muhimu kwa yeyote anayetaka kufaulu. Jitume sana na utathmini hatua unazopiga mara kwa mara. Pania mno kuboresha kesho yako na uombe Mola akuzidishie baraka zake.

Huu ndio ushauri wa Bw Yusuf Wambugu – mshairi shupavu, mwalimu mzoefu, mhasibu mzoefu na mwandishi hodari ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Kiswahili na mhariri wa habari katika runinga ya TV47 inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU).

Maisha ya awali

Wambugu alizaliwa mnamo 1978 katika kijiji cha Thumaita, eneo la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga. Ni mwanambee katika familia ya watoto watatu wa kiume wa Bw Benson Muchira na Bi Sheila Wambui.

Alisomea katika shule ya chekechea ya Thumaita mnamo 1985 kabla ya kujiunga na shule iyo hiyo kwa masomo ya msingi. Hii ilikuwa kati ya mwaka wa 1986 na 1994.

Hali ngumu ya kiuchumi na kimaisha ilimfanya kutumia muda zaidi kuhitimu masomo yake ya msingi. Alilazimika kufanya mtihani wa KCPE mara mbili kutokana na uchechefu wa fedha.

Alijiunga na Shule ya Upili ya Mutige katika kaunti ndogo ya Kirinyaga Mashariki mnamo 1995 na akahitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 1998.

Japo hakufaulu kujiunga na chuo kikuu moja kwa moja, anasema aliridhia alama alizopata kwani pako padogo si pakubwa pa mwenzako!

Mwalimu wake wa Kiswahili katika shule ya upili na ambaye kwa sasa ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Iribemwangi, alimchochea Wambugu kukichapukia Kiswahili. Anasema umahiri na ufasaha katika kufunza na kusema Kiswahili kwa mwalimu huyu hakukumithilika kabisa.

Japo Wambugu alipenda sana Kiswahili, akilini hakuwa na mwelekeo kamili wa taaluma ambayo angetaka kuizamia ukubwani. Hili ni jambo lililoishia kuwa mtihani mgumu zaidi uliozua vita ndani ya nafsi yake, asijue kabisa taaluma aliyotaka kuizamia maishani.

Ualimu

Wambugu alijiunga na chuo cha mafunzo ya ualimu cha Moi, Baringo mnamo 2000 na kuhitimu miaka miwili baadaye. Akiwa huko, alikutana na mwalimu gwiji Bi Audi aliyevusha mapenzi yake ya Kiswahili hadi ng’ambo nyingine.

Hapo chuoni, Wambugu alianzisha Chama cha Uanahabari na akazamia uandishi na utangazaji wa matukio ya mara kwa mara pale chuoni akiwa na wenzake Bernard Rono kutoka Bomet na Meme Naftaly kutoka Meru. Wakati huo, Wambugu alikuwa na mazoea ya kuiga sauti ya aliyekuwa mtangazaji maarufu wa Radio Citizen, marehemu Waweru Mburu.

Kati ya 2004 na 2010, Wambugu alikuwa mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Stepping Stones, Thika. Ufunzaji wake ulimvunia jina kubwa na wanafunzi wake wakaongoza katika mitihani ya kitaifa ndani na nje ya gatuzi zima la Kiambu. Kweli jina jema hung’aa gizani!

Kwa wakati huo wote, bado alikuwa akiandika miswada ya hadithi fupi, masuala ya sarufi, mashairi na makala maalum.

Uhasibu

Haja ya kubadilisha mkondo wa maisha pamoja na msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ni kati ya mambo yaliyomchochea Wambugu kujitosa katika ulingo wa uhasibu. Anaamini kwamba hakuna ziada mbovu.

Kati ya 2005 na 2009, alisomea uhasibu katika Taasisi ya Excel mjini Thika na kuhitimu kuwa mhasibu wa umma aliyeidhinishwa (CPA-K). Kwa sasa yeye ni mwanachama wa Taasisi ya Mahasibu Nchini Kenya (ICPAK).

Alisomea Shahada ya Usimamizi wa Biashara (BBM) katika Chuo Kikuu cha MKU kati ya 2010 na 2014. Alijisajili baadaye kwa Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara kitengo cha Fedha (MBA-FINANCE) katika Chuo Kikuu cha JKUAT na kufuzu mwaka wa 2019.

Baada ya kuhitimu kuwa mhasibu wa kiwango cha CPA-K, Wambugu alianza kufanya kazi ya uhasibu katika Chama cha Ushirika cha Wakulima cha Muki eneo la Kinangop, Kaunti ya Nyandarua mnamo 2011. Huo ni wadhifa ambao aliushikilia hadi mwaka wa 2013. Hatimaye alijiunga na Chuo kikuu cha MKU na kuwa Mkaguzi wa Ndani wa Hesabu kati ya 2014 na 2018.

Uanahabari

Mnamo Januari 2019, Wambugu alitoka katika ofisi ya ukaguzi wa hesabu na kujiunga na kitengo cha Kiswahili katika runinga ya TV47.

Hii ni baada ya pendekezo la Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Chuo Kikuu cha MKU, Profesa Simon Gicharu aliyeamini kwamba Wambugu ni bora zaidi katika masuala ya Kiswahili na uanahabari.

Kwa sasa yeye ni Mkuu wa Kitengo cha Kiswahili na mhariri wa habari katika runinga hiyo iliyoko Parklands, Nairobi.

Uandishi

Wambugu alianza kuandika akiwa mbichi katika shule ya upili. Hapa ni pale alipojaribu kutunga mashairi na kuandika hadithi fupi akimuiga mwalimu wake wa Kiswahili.

Hata hivyo, uandishi wake ulianza kunawiri akiwa katika chuo cha mafunzo ya ualimu na alipokuwa mwalimu wa Kiswahili shuleni Stepping Stones. Alizamia uandishi wa mada tofauti tofauti na tanzu mbalimbali za fasihi. Aliandika hadithi fupi, mashairi, hadithi za watoto na vitabu vya sarufi.

Zaidi ya kuwasilisha makala ya kitaaluma katika makongamano tofautitofauti ya ualimu na uhasibu, Wambugu amekuwa pia akiandika mashairi na kuyaghani katika warsha za sampuli hiyo. Kuu zaidi ni katika makongamano ya kila mwaka ya wahasibu ambapo amewasilisha makala mara tatu. Kadhalika, aliwasilisha shairi na makala katika Kongamano la Kimataifa la Chama Cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA) katika Chuo Kikuu cha MKU mnamo 2017.

Kwa wakati wote aliofanya kazi ya uhasibu, alikuwa akichangia mashairi katika gazeti la Taifa Leo na hata akaangaziwa katika ukumbi wa ‘Mshairi Wetu’.

Alijichapishia kwanza kitabu chake cha hadithi chenye anwani ‘Dunia ya Pili na Hadithi Nyingine’. Hiki kilifuatwa na novela ‘Kilio Kikavu’ na kamusi ya watoto iitwayo ‘Tufahamu Wanyama, Ndege na Wadudu’ vitabu vyote vikichapishwa na Kampuni ya Chania Publishers.

Kitabu ‘Kigezo cha Sarufi na Insha kwa Shule za Msingi’ kilichochapishwa majuzi na Chania Publishers ni mwongozo maridhawa kwa watahiniwa wa mitihani ya kitaifa ya KCPE. Kazi yake ya mwisho kuchapishwa ni hadithi ya watoto inayohimiza utunzaji wa mazingira, ‘Swala Mtoro na Mwanawe’.

Jivunio

Wambugu ni mumewe Bi Jackline Kalunda na baba ya watoto watatu wa kiume: Frankline, Tony na Caleb.

Anajivunia kuwa kielelezo chema kwa wanataaluma wa uhasibu wanaopenda Kiswahili kama vile Makokha Wanjala. Anastahi sana Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Mount Kenya, Prof Simon Gicharu kwa kutambua umilisi, ufasaha na weledi wake katika Kiswahili.