Haaland abeba Borussia Dortmund dhidi ya Union Berlin ligini

Na MASHIRIKA

ERLING Braut Haaland alifunga mabao mawili na kufikisha idadi ya magoli yake hadi saba kutokana na mechi tano za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Magoli hayo ya Haaland mnamo Jumapili yalisaidia waajiri wake Borussia Dortmund kucharaza Union Berlin 4-2 ligini. Haaland ambaye ni raia wa Norway, alifungia Dortmund bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya Berlin kutoka nyuma kwa mabao 3-0.

Raphael Guerrero aliwaweka Dprtmund uongozini mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Haaland kufunga la pili na Marvin Friedrich kujifunga na kufanya mambo kuwa 3-0.

Hata hivyo, penalti ya Max Kruse na bao jingine kutoka kwa Andreas Voglsammer yalitosha kurejesha Berlin mchezoni. Ingawa hivyo, Haaland alizima ghafla matumaini ya wageni wao dakika saba kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Nyota huyo aliyesajiliwa kutoka RB Salzburg ya Austria mnamo Januari 2020, sasa anajivunia mabao 68 kutokana na mechi 67 ambazo amechezea Dortmund katika mapambano yote.

Dortmund kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Bundesliga kwa alama 12, moja pekee nyuma ya viongozi Wolfsburg na Bayern Munich. Dortmund wameshinda mechi nne kati ya tano za ufunguzi wa muhula huu japo wamefungwa angalau mabao mawili katika kila mojawapo ya mechi hizo.

Matokeo ya Bundesliga (Septemba 19, 2021):

Dortmund 4-2 Union Berlin

Stuttgart 1-3 Leverkusen

Wolfsburg 1-1 Frankfurt

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO