Haaland afunga hat-trick ya nne katika mechi 19 za EPL na kufikisha jumla ya mabao 31 akichezea Man-City

Haaland afunga hat-trick ya nne katika mechi 19 za EPL na kufikisha jumla ya mabao 31 akichezea Man-City

Na MASHIRIKA

ERLING Haaland alifunga mabao matatu katika mechi moja (hat-trick) kwa mara ya nne msimu huu wa 2022-23 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kufikisha jumla ya mabao 31 katika mashindano yote ambayo amesakatia Manchester City waliokomoa Wolverhampton Wanderers 3-0 mnamo Jumapili ugani Etihad.

Kati ya mabao hayo ya Haaland, 25 yametokana na michuano 20 ya EPL muhula huu tangu abanduke kambini mwa Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Baada ya kukomesha ukame wa mabao kutokana na mechi tatu kwa kufunga dhidi ya Tottenham Hotspur ligini mnamo Januari 19, 2023, Halaand ambaye ni raia wa Norway, alihitaji dakika 12 pekee kusambaratisha kabisa mipango ya Wolves.

Aliwaweka mabingwa watetezi Man-City uongozini mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na Kevin de Bruyne. Alianza kipindi cha pili kwa matao ya juu na akafunga penalti iliyotokana na Ilkay Gundogan kuchezewa visivyo na nahodha Ruben Neves kabla ya kukamilisha krosi ya Riyad Mahrez na kuacha hoi kipa Jose Sa.

Mabao 25 ya Haaland ni matano zaidi kuliko yaliyofungwa na Luis Suarez mnamo 2013-14 alipoweka rekodi ya idadi kubwa zaidi ya magoli kufikia nusu ya msimu wa EPL.

Magoli ya sasa ya Haaland yangetosha kumzolea taji la mfungaji bora wa EPL katika zaidi ya nusu ya misimu 30 iliyopita tangu Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza ianze kuitwa EPL mnamo 1992.

Kwa kufunga mabao matatu dhidi ya Wolves, Haaland alimpiku Mohamed Salah na kufikia theluthi ya hat-tricks 12 zilizowahi kufungwa na kigogo raia wa Argentina, Sergio Aguero, akivalia jezi za Man-City katika EPL.

Ni nguli Alan Shearer (tano) anayejivunia kufunga hat-trick nyingi zaidi katika msimu mmoja wa EPL.

Taji la mwisho kwa Haaland kunyanyua ligini ni miaka mitatu iliyopita nchini Austria. Kombe lake la mwisho kutwaa ni la German Cup akivalia jezi za Dortmund ya Ujerumani mnamo 2021.

Ushindi wa Man-City dhidi ya Wolves uliwadumisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 45, tano nyuma ya viongozi Arsenal waliotandika Manchester United 3-2 ugani Emirates mnamo Jumapili.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Leeds 0-0 Brentford

Man-City 3-0 Wolves

Arsenal 3-2 Man-United

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

‘Nipe nikupe’ ya Ruto na Raila yaendelea

Vihiga Queens na Nakuru City Queens wapigana vita vikali...

T L