Haaland aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao UEFA baada ya kucheka na nyavu mara tano na kuongoza Man-City kudhalilisha Leipzig ugani Etihad

Haaland aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao UEFA baada ya kucheka na nyavu mara tano na kuongoza Man-City kudhalilisha Leipzig ugani Etihad

NA MASHIRIKA

ERLING Haaland aliweka historia kwa kufunga mabao matano katika ushindi mnono wa 7-0 uliosajiliwa na Manchester City dhidi ya RB Leipzig ya Ujerumani mnamo Jumanne usiku na kufuzu kwa robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Nyota huyo raia wa Norway sasa ndiye mchezaji mchanga zaidi katika historia kuwahi kufikisha mabao 30 haraka zaidi kwenye soka ya UEFA.

Aidha, ndiye mwanasoka chipukizi zaidi kuwahi kufunga mabao matano katika pambano moja la UEFA, hivyo kufikia rekodi za awali za masupastaa Lionel Messi wa Argentina na aliyekuwa fowadi mzoefu wa Brazil, Luiz Adriano.

Kufikia sasa, Haaland, 22, anajivunia mabao 39 kutokana na mechi za mashindano yote msimu huu. Ndiye mchezaji wa kwanza wa Man-City kuwahi kufikisha idadi hiyo ya mabao katika kampeni za msimu mmoja. Mabao matatu katika kila mojawapo ya mechi tano (hat-tricks tano) anazojivunia ni tatu zaidi kuliko ambazo zimewahi kufungwa na mchezaji yoyote katika Ligi Kuu tano za bara Ulaya; yaani EPL (Uingereza), La Liga (Uhispania), Bundesliga (Ujerumani), Ligue 1 (Ufaransa) na Serie A (Italia).

Mabao mengine ya Man-City yalijazwa kimiani na Ilkay Gundogan na Kevin de Bruyne katika kipindi cha pili na hivyo kusaidia mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kudengua Leipzig kwa jumla ya mabao 8-1.

Ushindi wa 7-0 uliosajiliwa na Man-City dhidi ya Leipzig ugani Etihad ulirejesha kumbukumbu za mwaka wa 2019 ambapo masogora hao wa kocha Pep Guardiola walidhalilisha pia Schalke ya Ujerumani katika kipute cha UEFA.

Ilivyo, dalili zote zinaashiria kiu ya Guardiola kunyanyulia Man-City taji la UEFA msimu huu na ushindi wao ni onyo kali dhidi ya wapinzani watakaokutana nao kwenye robo-fainali baada ya droo kufanyika Machi 17, 2023.

Hofu zaidi kwa sasa ni kwa nahodha wa zamani wa Man-City, Vincent Kompany, anayejiandaa kuongoza kikosi chake cha Burnley kuvaana na masogora wa Guardiola katika robo-fainali za Kombe la FA mnamo Machi 18, 2023 ugani Etihad.

Kocha wa sasa wa Leipzig, Marco Rose, aliwahi kuwa mkufunzi wa Haaland msimu uliopita wa 2021-22 kambini mwa Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Man-City walishuka dimbani dhidi ya Leipzig wakiwa na kiu ya kumaliza kazi baada ya kutoshana nguvu na kikosi hicho kwa sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ugani Red Bull Arena mnamo Februari 22, 2023.

Sawa na Leipzig waliokomoa Borussia Monchengladbach 3-0 katika pambano lao la awali katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) nyumbani, Man-City nao walitarajiwa kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Crystal Palace katika EPL uwanjani Selhurst Park mnamo Machi 11, 2023.

Mechi dhidi ya Palace ilikuwa ya nne mfululizo kwa masogora hao wa Guardiola kushinda tangu wakabwe koo na Leipzig katika UEFA. Ushindi wa Jumanne usiku unaweka hai matumaini yao ya kujizolea jumla ya mataji matatu msimu huu kadri wanavyofukuzia ufalme wa UEFA kwa mara ya kwanza katika historia.

Mbali na kuhifadhi ubingwa wa EPL – kipute ambacho wamekitawala mara nne katika kipindi cha misimu mitano – Man-City wangali pia kwenye Kombe la FA.

Man-City walibanduliwa nje ya UEFA katika hatua ya 16-bora mara ya mwisho mnamo 2016-17 walipozidiwa ujanja na AS Monaco kwa wingi wa mabao ya ugenini baada ya sare ya 6-6. Msimu huo, walipepeta Monaco 5-3 ugani Etihad kabla ya kupigwa 3-1 kwenye marudiano nchini Ufaransa.

Kwa kuangusha Leipzig, Man-City sasa wamefikia rekodi ambayo imeshikiliwa na Arsenal kwa miaka 14 iliyopita – timu ya Uingereza ambayo haijawahi kupigwa katika idadi kubwa zaidi ya mechi za UEFA nyumbani.

Kufikia sasa, Man-City hawajashindwa katika mechi 24 za bara Ulaya ugani Etihad huku wakilaza wapinzani mara 22 kutokana na michuano hiyo. Miamba hao wameshinda mechi zote saba zilizopita ambazo wamechezea nyumbani katika mashindano yote tangu mkesha wa mwaka mpya wa 2023 walipoambulia sare ya 1-1 dhidi ya Everton katika EPL.

Ili kupokeza Man-City kichapo cha kwanza mwaka huu, kocha Rose wa Leipzig alikuwa na ulazima wa kuiga mbinu za Guardiola – mkufunzi wa mwisho kuwahi kuongoza kikosi cha Ujerumani kushinda mechi ya UEFA ugani Etihad akidhibiti mikoba ya Bayern Munich mnamo 2013-14.

Tangu wakati huo, majaribio 10 sasa ya vikosi vya Bundesliga kulaza Man-City ugani Etihad yameambulia patupu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wataja ruzuku ya bei ya unga wakati wa Uhuru kuwa...

BORESHA AFYA YAKO: Mbaazi ni mlo mtamu wenye faida tele kwa...

T L