Haaland aweka rekodi ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kufunga mabao 50 katika Bundesliga

Haaland aweka rekodi ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kufunga mabao 50 katika Bundesliga

Na MASHIRIKA

ERLING Braut Haaland aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kufikisha mabao 50 katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya kuongoza waajiri wake Borussia Dortmund kupepeta Wolfsburg 3-1 mnamo Jumamosi.

Akiwa na umri wa miaka 21 na siku 129, bao la Haaland dhidi ya Wolfsburg lilikuwa lake la 10 ndani ya jezi za Dortmund kutokana na mechi saba zilizopita baada ya jeraha kumweka nje ya michuano kadhaa mnamo Oktoba. Baada ya kushinda mechi sita kati ya saba za Bundesliga, Dortmund kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 30, moja nyuma ya mabingwa watetezi Bayern Munich waliocharaza Arminia Bielefeld 1-0.

Bao ambalo Bayern walifungiwa na Leroy Sane liliwawezesha kuvunja rekodi ya miaka 44 katika soka ya Ujerumani. Miamba hao kwa sasa wamefunga magoli 102 mnamo 2021 na kupiku Cologne waliopachika wavuni mabao 101 mnamo 1977.

Dortmund walikung’uta Wolfsburg siku tatu baada ya kichapo cha 3-1 kutoka kwa Sporting Lisbon ya Ureno kuwadengua kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

You can share this post!

Atalanta yapiga Juventus nyumbani kwa mara ya kwanza tangu...

Liverpool waweka rekodi katika soka ya Ligi Kuu ya...

T L