Michezo

Haaland kukosa fainali za Euro baada ya Serbia kubandua Norway kwenye mchujo

October 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

SERBIA watakutana sasa na Scotland kwenye mechi nyingine ya kufuzu kwa fainali za Euro mwaka ujao baada ya bao la dakika za mwisho kutoka kwa Sergej Milinkovic-Savic kuwasaidia kuwabandua Norway kwenye mchujo wa nusu-fainali.

Milinkovic-Savic ambaye ni kiungo wa Lazio alifunga bao la kwanza katika dakika ya 81 kabla ya kupachika wavuni la pili katika muda wa ziada na kuzamisha chombo cha Norway waliosawazishiwa na Mathias Normann katika dakika ya 88.

Kichapo ambacho Norway walipokezwa kinamaanisha kwamba chipukizi wa Borussia Dortmund, Erling Haaland sasa hatakuwa sehemu ya nyota watakaonogesha kivumbi cha Euro mwaka 2021.

Scotland walijikatia tiketi ya kuvaana na Serbia baada ya kuwadengua Israel kwa penalti 5-3 baada ya mchuano wao kukamilika kwa sare tasa uwanjani Hampden Park, Scotland mnamo Oktoba 8, 2020.