Makala

SHINA LA UHAI: Habari feki zilizogubika homa ya Corona – WHO

February 11th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

TANGU kutokea kwa mkurupuko homa ya Corona kumekuwa na taarifa tele za kupotosha ambazo zimekuwa zikisambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

Miongoni mwa taarifa hizo ni madai kwamba maambukizi ya virusi hivyo yanaweza kutokana na barua au mzigo kutoka China.

Lakini Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa virusi hivyo haviambukizwi kupitia mizigo au bahasha.

“Virusi vya Corona vinakufa haraka vinapokuwa nje ya mwili. Hivyo, haviwezi kutoka China hadi Kenya, kwa mfano, vikiwa hai,” linasema shirika hilo.

WHO linasema kuwa hakuna ushahidi kwamba virusi hivyo vinaweza kuenezwa kutoka kwa mifugo wa nyumbani kama vile paka na mbwa hadi kwa binadamu.

Lakini linashauri kuwa ni vyema unawe mikono baada ya kugusa mifugo hao ili kujikinga na bakteria kama vile E.coli na Salmonella ambao husababisha kuhara. Bakteria hao husambaa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu.

Wataalamu wanasema kuwa chanjo dhidi ya maradhi ya homa ya mapafu (nimonia) haiwezi kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

“Virusi vinavyosababisha homa ya Corona ni vipya kabisa na vinahitaji chanjo yake. Wanasayansi wanaendelea kufanya utafiti ili kubaini chanjo ya kuzuia maradhi hayo,” linasema shirika la WHO.

Madaktari pia wanasema kuwa kuosha pua au mdomo mara kwa mara hakuwezi kumsaidia mtu kuepuka maambukizi ya virusi hivyo.

“Kuna baadhi ya kemikali za kuoshea mdomo ambazo zinaua bakteria kwenye mate kwa muda mfupi na kisha kurejea tena. Kemikali hizo haziwezi kuua virusi vya Corona,” linasema WHO.

Linasema kuwa taarifa kwamba kitunguu saumu kinaweza kuua virusi vya Corona zinapotosha.

“Kitunguu saumu kina viungo ambavyo huua baadhi ya viini. Hata hivyo, hakuna ushahidi kwamba kina uwezo wa kuua virusi vya Corona. Kadhalika hakuna kemikali zozote au dawa ambayo imethibitishwa kuwa ina uwezo wa kuua virusi hivyo,” linasema.

Katika mitandao ya kijamii kumekuwa na madai kwamba virusi vya Corona vinaathiri watu wazima tu.

Lakini WHO linasema kuwa wote kuanzia watoto hadi wazee wako katika hatari ya kuambukizwa maradhi hayo bila kuzingatia umri.

Wagonjwa wa pumu, kisukari na maradhi ya moyo huwa kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha yao wanapoambukizwa virusi, kwa mujibu wa WHO.

Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia dawa za kukabiliana na bakteria (antibiotics) kama njia mojawapo ya kujilinda dhidi ya homa hii.

“Dawa za bakteria hazina uwezo wa kuua virusi. Homa ya Corona inasababishwa na virusi, hivyo dawa za kuua bakteria haziwezi zikakusaidia. Lakini pia inawezekana kwa mgonjwa kuambukizwa bakteria na virusi kwa pamoja,” linasema.

WHO lilitoa ufafanuzi huo baada ya kundi la watu kudai kupitia mitandao ya kijamii kwamba kemikali ambazo watu wamekuwa wakitumia kuchubua rangi ya ngozi inatibu ugonjwa huo.

Madai kwamba virusi vinasambaa kooni ndani ya dakika 10 iwapo watu hawatakunywa maji ya kutosha yamekuwa yakisambazwa kupitia mtandao wa WhatsApp katika Milki ya Falme za Urabuni (UAE).

Lakini WHO linashikilia kuwa madai hayo si ya kweli kwani homa hiyo bado haina tiba wala kinga.

Kampuni ya Facebook wiki iliyopita ilitangaza kuwa itaondoa kwenye mitandao yake; Facebook, Twitter na Instagram taarifa zote za kupotosha kuhusiana na ugonjwa wa huo.

Mtandao wa TikTok unaomilikiwa na kampuni ya Bytedance ya China, ulisema kuwa utaondoa taarifa zote zinazopotosha kuhusiana na chanjo na tiba ya homa ya Corona.