• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Kioni ataka mazungumzo baina ya Kenya Kwanza na Azimio yasitishwe mara moja

Kioni ataka mazungumzo baina ya Kenya Kwanza na Azimio yasitishwe mara moja

Na JAMES MURIMI

KATIBU Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ametaka kusitishwa kwa mazungumzo ya maridhiano kati ya wawakilishi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga na wale wa Rais William Ruto, akiyataja kama shughuli ya “kupoteza wakati.”

Akiongea na Taifa Leo Alhamisi, Septemba 21, 2023, Bw Kioni alisema Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo inayoendesha vikao vyake katika ukumbi wa Bomas of Kenya haitaibua suluhu kwa shida za kiuchumi zinazowakumba Wakenya.

Alisema mazungumzo hayo hayathaminiwi na utawala wa Kenya Kwanza ambao anasema haina nia ya kushughulikia masuala makuu yaliyoibuliwa na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

“Sitarajii kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda yoyote. Sote tunazungushwa tu na hivyo shughuli hiyo ni ya kupoteza wakati,” Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragua akasema kupitia mahojiano kwa njia ya simu.

“Ukisikia matamshi ya kuvunja moyo kutoka kwa viongozi wa Kenya Kwanza kuhusu hali ya kiuchumi, basi utagundua kuwa mazungumzo hayo hayana maana,” akaongeza.

Alisuta utawala wa Rais Ruto kama uliosheni viongozi wajeuri na ambao wamefeli kupunguza bei ya mafuta na bidhaa nyinginezo za kimsingi.

“Kuna hatua madhubuti zinazopasa kuchukuliwa kufufua uchumi wetu. Viongozi hawafai kuonyesha ujeuri kwa Wakenya wenye njaa na hasira. Hatutakubali kuhadaiwa,” Bw Kioni akasema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter amemtaka Rais Ruto kuvunja baraza lake la mawaziri, akisema mawaziri wa sasa hawajali hali ngumu ya kiuchumi inayowakumba Wakenya.

“Baadhi ya Maafisa Wakuu wa Serikali wamekuwa wajeuri badala wa kuwahurumia wananchi. Tunagharamia mafuta ambayo magari yao hutumia, ilhali wanadiriki kutuzomea na kututusi tukilalamikia kupanda kwa bei ya mafuta. Hawafai kufanya hiyo,” Bw Keter akaambia Taifa Leo.

Haya yanajiri wakati ambapo Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ametoa wito kwa upinzani kukoma kuhujumu mazungumzo yanayoendelea Bomas of Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Kilio Man-U, Arsenal ikipiga sherehe Uefa

Mwaka 1 hatujaonana na anadai ana mimba yangu

T L