NA TITUS OMINDE
MAMA mwenye umri wa miaka 26 anayeshtakiwa kwa kumdunga kisu na kumuua mwanawe wa miaka miwili, atazuiliwa kwa siku 21 hadi uchunguzi utakapokamilika.
Mwanamke huyo, Charistable Jepkosgei pia anakabiliwa na shtaka la kumjeruhi vibaya bintiye wa miaka sita, akijitetea katika Mahakama ya Eldoret kwamba msukumo wa tukio hilo la kinyama ulitokana na ugomvi wa kinyumbani baada ya kuachana na mumewe.
Hakimu Mkuu Mwandamizi Richard Odenyo aliamuru mshukiwa azuiliwe katika seli za kituo cha polisi cha Eldoret Central kwa muda wa majuma matatu, kusubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi.
Akiwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa mshukiwa kupitia hati ya kiapo iliyowasilishwa kortini, afisa wa uchunguzi Koplo Edward Ndemo, anayehusishwa na idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), Kaunti Ndogo ya Turbo, alisema bado hajakamilisha uchunguzi.
Bw Ndemo aliambia mahakama kwamba polisi bado hawajarekodi taarifa kutoka kwa mashahidi wakuu.
Mbali na kukamilisha uchunguzi, mshukiwa huyo anapaswa kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi wa kiakili kabla kufunguliwa mashtaka.
“Tunataka kumpeleka mwanamke huyo katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi kwa uchunguzi wa kiakili ili kubaini iwapo yuko sawa kujibu mashtaka ya mauaji. Pia tunataka kuchukua sampuli ya damu kutoka kwake na kisu alichotumia katika mauaji ya mwanawe kifanyiwe uchunguzi wa kitaalamu katika maabara ya serikali,” alisema Bw Ndemo.
Alifahamisha mahakama iliyojaa watu kwamba mvulana aliyeuawa alizikwa siku hiyo hiyo aliyokumbana na mauti, kulingana na sheria za Kiislamu akiongeza kwamba mwanawe wa kike bado anapigania maisha yake katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi.
Bi Jepkosgei anadaiwa kumdunga mwanawe shingoni kwa kutumia kisu cha jikoni na kusababisha kifo chake katika nyumba yake ya kukodisha mtaa wa West Indies, viungani mwa mji wa Eldoret.
Alipokuwa akijibu ombi la kuzuiliwa kwa siku 21, alikiri kumuua mwanawe, akihusisha kitendo hicho kiovu na msongo wa mawazo na mafadhaiko anayopitia.
“Sikuwa na nia ya kumdhuru mtoto wangu yeyote ambaye nilimpenda sana lakini nililazimika kumuua mwanangu kutokana na msongo wa mawazo na mateso ambayo napitia mikononi mwa baba yao,” aliambia mahakama.
Kesi hiyo itatajwa mnamo Juni 19, 2023.