• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Aliyekuwa msimamizi wa ikulu aombolezwa

Aliyekuwa msimamizi wa ikulu aombolezwa

Na BENSON MATHEKA

ALIYEKUWA msimamizi wa Ikulu, Abrahamu Kiptanui, alifariki dunia Jumapili baada ya kulazwa hospitalini kwa mwezi mmoja.

Kulingana na familia yake, Kiptanui alifariki jana asubuhi katika Nairobi Hospital ambako amekuwa akitibiwa.

Familia ilieleza kwamba, Kiptanui aliyekuwa msimamizi wa ikulu wakati wa utawala wa Hayati Daniel Moi alikuwa ameugua kwa muda mrefu.

Chini ya utawala wa Moi, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa na ushawishi mkubwa.

Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga walikuwa miongoni mwa waliomwomboleza Kiptanui wakisema alikuwa mtumishi wa umma aliyekuwa na bidii katika kazi yake.

“Abraham Kiptanui, aliyekuwa msimamizi wa ikulu alitumikia nchi hii kwa unyenyekevu na kujitolea. Alikuwa afisa wa utawala asiyechoka kutekeleza majukumu yake,” alisema Dkt Ruto.

Bw Odinga alimtaja marehemu Kiptanui kama mtaalamu aliyesaidia Moi kuunganisha nchi wakati wa changamoto nyingi.

Naye seneta wa Baringo Gideon Moi alisema alipokea habari za kifo cha Kiptanui kwa huzuni.

“Natuma rambirambi zangu kwa familia kwa pigo hili la uchungu na ninawahakikishia usaidizi wangu na maombi wakati huu mgumu wa majonzi,” alisema.

Mbunge wa Ainabkoi William Chepkut alimtaja marehemu Kiptanui kama mzalendo mkuu na mtetezi wa watu.

“Alikuwa kiongozi mnyenyekevu. Naombea familia yake,” aliomboleza Chepkut

Kiptanui alistaafu mwaka wa 1996. Familia yake ilisema kwamba itatangaza tarehe ya mazishi baadaye.

You can share this post!

Wauzaji watoroka ada nyingi za kaunti

BI TAIFA APRILI 5, 2021