• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Ashtakiwa kwa kuua mpenzi wake chuoni     

Ashtakiwa kwa kuua mpenzi wake chuoni    

 

NA TITUS OMINDE

MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Eldoret (UOE) anayeshukiwa kumuua mpenziwe wiki tatu zilizopita amezuiliwa kwa siku sita ili kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi.

Mnamo Alhamisi mahakama ya Eldoret iliruhusu wapelelezi kumzuilia Kenneth Kibet, 24, kufuatia ombi la maafisa wa uchunguzi.

Alipokuwa akiwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa mshukiwa, mchunguzi wa kesi hiyo Edward Ndemo aliambia mahakama kuwa mshtakiwa alikamatwa Mei 1, 2023 na kupelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi kwa matibabu baada ya kujaribu kujitoa uhai.

Hati za mashtaka mahakamani zilionyesha kuwa Bw Kibet alimuua mpenziwe, Sheila Jemutai kabla ya kujaribu kujitia kitanzi kwa kile polisi walitaja kuwa mzozo wa kimapenzi.

Tangu kukamatwa kwake, amekuwa hospitalini akipokea matibabu kabla ya kuruhusiwa kuondoka.

Kulingana na wapelelezi, mshtakiwa alitumia kisu cha jikoni kutekeleza kitendo hicho kiovu katika nyumba ya kupangisha ya marehemu katika kituo cha biashara cha Sogomo karibu na chuo hicho.

Tukio hilo lilitokea Mei 1, 2023 ambapo alikuwa ametembelea mpenzi wake.

Ingawa Bw Ndemo aliomba korti muda wa siku 14, mahakama ilichagua siku sita ikisisitiza kuwa polisi walikuwa na muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi wakati mshukiwa alikuwa akipokea matibabu hospitalini.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Eldoret Richard Odenyo aliamuru mshukiwa azuiliwe katika seli za kituo kikuu cha polisi cha Eldoret kwa siku sita.

“Baada ya kutafakari kwa makini maombi yaliyowasilishwa na polisi ambapo mshukiwa hajayapinga, naona kuna sababu za msingi za kuamuru kumwekwa kizuizini,” aliamuru hakimu.

Aliagiza polisi wawasilishe mshukiwa mahakamani Mei 30, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa kutumia magari ya watu kuchukua mikopo

‘Ker’ mpya wa jamii ya Waluo kujulikana baada...

T L