• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Askofu alalamikia kulazimishwa kubeba kinyesi akiwa seli kwa kesi ya ulanguzi wa watoto

Askofu alalamikia kulazimishwa kubeba kinyesi akiwa seli kwa kesi ya ulanguzi wa watoto

Na RICHARD MUNGUTI

MUHUBIRI wa kimataifa Askofu Gilbert Juma Deya anayeshtakiwa kuiba na ulanguzi wa watoto watano jana alijitetea akisema yeye ni mueneza injili na hahusiki kamwe na biashara hiyo.

“Mimi sikuhusika kamwe na wizi wa watoto. Sijawahi kushiriki ama kuhusika na kashfa ya ulanguzi wa watoto,” Askofu Deya alimweleza hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Robison Ondieki.

Alisema katika kesi inayomkabili, serikali haikumletea mtoto hata mmoja kortini kuthibitisha madai alihusika na wizi wa watoto.

Askofu Deya alieleza mahakama watoto wake ni wawili aliojaliwa pamoja na mkewe aliyemtaliki Mary Deya.

“Kesi hii niliyoshtakiwa ni fitina tupu na haina msingi wowote. Naomba korti iniachilie huru na kusafisha jina langu katika kashfa hii mbaya,” Askofu Deya alisema akijitetea.

Pia alieleza mahakama hakuna mzazi hata mmoja aliyefika kortini kudai “niliiba mtoto wake.”

Mhubiri huyo maarufu wa televisheni nchini Uingereza alimweleza Bw Ondieki kwamba mkewe-Mary Deya- ndiye alishtakiwa kwa wizi wa watoto lakini akaachiliwa na mahakama kuu.

“Tangu mwaka wa 1995 sikurudi Kenya kwa vile nilikuwa nahofia maisha yangu. Sifa mbaya zangu zilienezwa kote ulimwenguni kwamba nilikuwa muuaji, mlanguzi na muuzaji wa watoto na hivyo nikaogopa kurudi Kenya,” Askofu Deya aliambia mahakama.

Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili John Swaka na kuhojiwa na viongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku na Hellen Mutellah, Askofu Deya alieleza korti ilibidi aishtaki serikali ya Kenya Uingereza kulinda haki zake.

“Mahakama kuu ya Westminister iliizuia serikali ya Kenya kunirudisha nchini kunifungulia mashtaka baada ya aliyekuwa mke wangu kuachiliwa huru na kuondolewa lawama za wizi wa (watoto waliozaliwa kimiujiza),”Askofu Deya alisema.

Aliishangaza mahakama aliposema ilibidi abebe kinyesi chake kwa ndoo alipozuiliwa katika kituo kimoja cha polisi.

Aliambia mahakama aliteswa bure na yuko na hakika kwamba “hana makosa na anastahili kuachiliwa huru.”

Kesi itaendelea Mei 31.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge washangazwa na ununuzi wa stima kutoka Rerec

Afueni kwa waziri wa zamani akiondolewa kesi ya ufisadi wa...

T L