• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Bondia Okwiri kupigania mamilioni Agosti, Mike Tyson atakuwepo pia Nairobi

Bondia Okwiri kupigania mamilioni Agosti, Mike Tyson atakuwepo pia Nairobi

Na AYUMBA AYODI

Bingwa wa taji la Afrika (ABU) la uzani wa kati Rayton “Boom Boom” Okwiri amesaini kandarasi ya miaka mitano na mapromota wa masumbwi wa Raynelo kutoka Amerika.

Bondia huyo Mkenya kutoka Idara ya Magereza alifichua Jumanne kuwa makubaliano hayo yatashuhudia akipokea Sh5 milioni (Dola 50,000) kwa kila pigano la taji na Sh1 milioni (Dola 10, 000) kwa kila pigano lisilo la kuwania taji. Raynelo inapanga kumtafutia angaa mapigano matano kila mwaka.

Okwiri, ambaye alisherehekea kufikisha umri wa miaka 35 mnamo Mei 26, alifanya mapatano na mmiliki wa Raynelo, Nelson Lopez Junior baada ya kuwasili mjini Florida hapo Mei 29.

“Nadhani ni dili nzuri kwangu kwa sababu ameahidi kuhakikisha kuwa mapigano yangu kadhaa yanapeperushwa kwenye runinga, kitu ambacho naamini huenda kikaimarisha umaarufu wangu nikipata ushindi,” alisema Okwiri ambaye anajiandaa kwa pambano lake la kwanza la taji la Shirika la Ndondi Duniani (WBO) litakalofanyika mjini Nairobi mwezi Agosti 2021.

Pigano hilo la Okwiri ndilo litakuwa kubwa la kampuni ya kamari ya 22Bet. Bingwa wa zamani wa dunia wa uzani wa “Heavy” Mike “Iron Mike” Tyson atakuwepo kushiriki pigano la maonyesho.

“Mimi sikutupilia mbali mazoezi wakati michezo ilisitishwa mwezi Machi mwaka jana kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona,” alisema Okwiri ambaye alikuwa amerejea kushiriki ndondi zisizo za malipo kujaribu kutafuta tiketi ya Olimpiki, lakini hakufaulu.Okwiri alishindwa kufuzu kupitia mashindano ya Bara Afrika yaliyoandaliwa Februari 2020.

Hata hivyo, Okwiri alisema anamakinia ndondi za malipo zaidi kuliko wakati mwingine maishani mwake akilenga kushinda mataji kadhaa kabla ya kustaafu.

“Nimesalia na miaka mitano ya kulimana ngumi na sina budi kujitolea kwa dhati kupata matokeo bora. Nimekuwa katika masumbwi tangu mwaka 2002 na umri wangu umeanza kunipa kisogo,” alisema Okwiri ambaye ameshinda mapigano matano na kutoka sare moja katika sita ameshiriki ya malipo.

  • Tags

You can share this post!

Maajabu mwanamke Afrika Kusini akivunja rekodi ya dunia...

Wolves wamteua kocha Bruno Lage kujaza pengo la mkufunzi...