• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Chuo Kikuu cha Mount Kigali chapata ‘miguu’ rasmi kujisimamia

Chuo Kikuu cha Mount Kigali chapata ‘miguu’ rasmi kujisimamia

NA LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kigali kimepewa kibali maalum cha utambulisho rasmi.

Mnamo Aprili 2023, baada ya kujiendeleza kwa miaka mitano, chuo hicho, ambacho kilianza kama bewa la Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) jijini Kigali, Rwanda kilikabidhiwa mikoba ya kujiendeleza kivyake.

Hafla hiyo ya kupata kibali kipya kuwa chuo cha kujitegemea ilihudhuriwa na mwanzilishi na mwenyekiti wa bodi ya MKU Prof Simon Gicharu, ambaye alisifu juhudi za kupandishwa hadhi Chuo Kikuu cha Mount Kigali.

Wakati wa sherehe hiyo, chuo hicho kilipewa muhuri aina ya seal na fimbo aina ya mace kama viashiria muhimu vya utambulisho.

Vifaa hivyo ni muhimu kwa chuo hicho kwa sababu ndivyo vibali maalum vya kukipa chuo nafasi ya kujisimamia na kuendesha mambo bila tashwishi.

Kulingana na mpangilio huo, chuo hicho kina nafasi ya kutuza wanaofuzu shahada za digrii, diploma na stashahada.

Wakati wa hafla hiyo katika eneo la Gatenga jijini Kigali, Prof Gicharu alikabidhi vifaa vyote vya utendakazi vya chuo hicho kwa Prof Stanley Waudo ambaye naye alimkabidha Dkt Innocent Mugisha ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya usimamizi.

Baadaye Dkt Mugisha alikabidhi vifaa hivyo vya utendakazi kwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Mount Kigali Dkt Martin Kimemia.

“Mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa karibu miongoni mwa wakuu wa chuo, wanafunzi, wazazi, na wahitimu,” alisema Prof Gicharu.

Dkt Mugisha naye alisema hii ni mara ya kwanza kwa chuo hicho kutambulika kama chuo kikuu nchini Rwanda.

“MKU imekuwa ikiweka hadhi ya mafunzo ya elimu ya juu kulingana na mwongozo wa kimataifa,” alisema Dkt Mugisha.

Wakati wa hafla hiyo, Wakfu wa Imbuto, Mireille Musaniwabo na Kagabo Innocent ambaye ni msajili wa Baraza la Kitaifa la Wauguzi na Wataalamu wa Kusaidia Wajawazito, walihudhuria.

Bi RoseAnne Muregwa aliyekuwa mwanafunzi wa chuo cha Kigali alimsifu Prof Gicharu kwa maono yake ya kuzindua chuo hicho.

Aidha Dkt Martin Kimemia alisema chuo hicho kitajisimamia bila shida.

Wakati huo pia chuo hicho kinajenga hoteli kubwa ya kifahari ambayo itawasajili wanafunzi wapya watakaofanya masomo ya utalii.

Wakati huo kituo cha afya kitazinduliwa kutoa huduma kwa wengi.

Dkt Kimemia alisema chuo hicho kimewekeza takriban Sh20 milioni za kununua vifaa vya matibabu ya meno vitakavyotumika kwa wanafunzi wanaojifunza udaktari wa meno na maswala mengine ya kiafya.

  • Tags

You can share this post!

Maafisa kadhaa wa KDF wapoteza maisha kwenye ajali ya ndege...

Visa vya mabweni kuteketea vyaongezeka

T L