• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Chuo Kikuu cha Mtandaoni kuzinduliwa rasmi mwezi huu, aahidi Rais Ruto

Chuo Kikuu cha Mtandaoni kuzinduliwa rasmi mwezi huu, aahidi Rais Ruto

NA CHARLES WASONGA

KUFIKIA mwishoni mwa mwezi huu wa Juni, Wakenya wataanza kusomea shahada za digrii kupitia mtandaoni kufuatia kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Huduma za Mtandaoni cha Kenya (Open University of Kenya).

Akiongea mnamo Alhamisi wakati wa maadhimisho ya 60 ya Madaraka Dei, kiongozi wa nchi alisema wakati huu kozi zinapakiwa mtandaoni na masomo hayo yatazinduliwa mwishoni mwa mwezi huu.

“Hatimaye Chuo Kikuu cha Mtandaoni kitaidhinishwa mwishoni mwa mwezi huu na sasa kozi zinapakiwa tayari kuzinduliwa,” akasema alipowahutubia Wakenya katika uwanja wa michezo wa Moi mjini Embu.

“Baada ya kuzinduliwa kwa masomo hayo, Wakenya wataweza kupata masomo ya vyuo vikuu kutoka majumbani mwao kwa kutumia vyombo vya teknolojia ya kisasa kama simu na tarakilishi,” Dkt Ruto akaongeza.

Chuo hicho kitaendesha shughuli zake kama taasisi nyingine ila mafunzo yatatolewa kupitia mtandaoni sio masomo ya ana kwa ana.

Mnamo Februari mwaka huu Wizara ya Elimu ilifichua baadhi ya kozi ambazi zitafundishwa katika Chuo Kikuu cha Mtandao.

Masomo ya chuo hicho yatashirikishwa na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Baadhi ya kozi zitakazofunzwa katika chuo hicho ni Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Usalama ya Kimtandaoni na Uchunguzi wa Kidijitali, Shahada ya Kwanza katika Teknolojia ya Elimu na Shahada ya Sayansi ya Data, miongoni mwa nyingine.

  • Tags

You can share this post!

Makundi sasa kupata mkopo wa Hasla

Jenerali Ogolla achapa kibarua cha kwanza katika Sherehe ya...

T L