• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
DCI: Baadhi ya miili Shakahola haikuwa na viungo muhimu

DCI: Baadhi ya miili Shakahola haikuwa na viungo muhimu

BRIAN OCHARO Na VALENTINE OBARA

POLISI wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) wamedai kuwa, baadhi ya miili iliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, haikuwa na viungo muhimu.

Licha ya mwanapatholojia mkuu wa serikali, Dkt Johansen Oduor, kusema wiki iliyopita kwamba miili 112 iliyochunguzwa ilikuwa na viungo vyote, polisi Jumatatu waliambia mahakama baadhi haikuwa na viungo.

Wamedai kuwa, wanaamini mhubiri wa Kanisa la New Life, Bw Ezekiel Odero, alishirikiana na Bw Paul Mackenzie, anayehusishwa na mauaji ya halaiki Shakahola, katika biashara haramu ya viungo vya binadamu.

Hayo yaliibuka huku Mahakama ya Milimani, Kaunti ya Nairobi, ikikubali ombi la polisi kumzuia Bw Odero kutumia akaunti zake 35 za benki na M-Pesa kwa siku 30. Mawakili wake wakiongozwa na Bw Cliff Ombeta, walikosoa uamuzi huo. Bw Odero anachunguzwa kwa madai mbalimbali ya uhalifu, ikiwemo ulanguzi wa pesa.

Kupitia kwa hati ya kiapo, afisa wa DCI, Bw Martin Munene, alisema inashukiwa wahubiri hao walipata pesa kutoka kwa biashara hiyo haramu mbali na kushawishi waumini kuuza mali zao zote kisha kupeleka pesa kanisani. Afisa huyo aliongeza kuwa, polisi wanashuku kuna watu wengine wengi waliohusika katika biashara ya viungo vya miili ya binadamu.

“Pasta Ezekiel Ombok Odero…alishukiwa kwa ulanguzi wa pesa haramu kwa sababu ya uhusiano wake na Pasta Paul Mackenzie. Hii ilikuwa ni baada ya makaburi ya halaiki iliyopatikana Shakahola kuhusishwa na Pasta Paul Mackenzie…ambaye anashukiwa kuhusika katika unyofoaji na ulanguzi wa viungo vya miili ya binadamu,” akasema mpelelezi huyo wa uhalifu wa kifedha.

Wakati upasuaji wa miili ulipokuwa ukifanywa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi, baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yalilalamikia kufungiwa nje.

Mashirika hayo yalitaka kuruhusiwa kuwa na wawakilishi kushuhudia upasuaji wa miili, lakini serikali ikakataa ombi lao. Hali sawa na hii ilishuhudiwa katika msitu wa Shakahola ambapo mashirika hayo pamoja na wanahabari walianza kuzuiwa kushuhudia ufukuaji wa miili.

Hatua hizo zilikashifiwa, ikihofiwa serikali ilikuwa na njama ya kuficha ukweli. Polisi wamedai kuwa, akaunti za benki za Bw Odero zimekuwa zikipokea kiasi kikubwa cha pesa zinazoshukiwa kuwa sehemu ya pesa haramu.

Miongoni mwa akaunti ambazo mhubiri huyo amezuiwa kutumia, ni nne zilizosajiliwa kwa jina la Kilifi International School iliyojengwa katika kiwanja cha kanisa lake. Akaunti nyingine 20 zimesajiliwa kwa jina la New Life Prayer Centre ambapo baadhi zinashikilia sarafu za pesa za kigeni ikiwemo shilingi ya Tanzania, dola, yuro, na pauni. Akaunti nne za benki ziko kwa jina la Bw Odero, sawa na nyingine saba za M-Pesa.

  • Tags

You can share this post!

Wataalamu: Ushuru mpya utaumiza raia

Arama akosoa wanaosuta ziara zake Nyamira

T L