• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Familia yalia mgonjwa wao kuachwa kwenye ambulansi bila matibabu akaishia kufariki

Familia yalia mgonjwa wao kuachwa kwenye ambulansi bila matibabu akaishia kufariki

NA LUCY MKANYIKA

FAMILIA moja katika eneo la Taveta, kaunti ya Taita Taveta inaomboleza kifo cha jamaa yao ambaye aliachwa bila huduma katika ambulensi katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Moi mjini Voi.

Mgonjwa huyo alisubiri kwa takriban saa moja ndani ya ambulensi katika hospitali hiyo mnamo Jumatano baada ya wahudumu katika idara ya huduma za dharura kudai kuwa hawakupokea taarifa kuhusu uhamisho wa mgonjwa kutoka hospitali ya Taveta.

Marehemu, aliyetambuliwa kama Agnes Mutuku, 35, alikuwa amekimbizwa kutoka Taveta ili kupata matibabu maalum.

Kulingana na shangazi yake, Maria Wakesho, marehemu alilazwa katika hospitali ya Taveta na matatizo ya sehemu yake ya uzazi siku ya Jumatano asubuhi lakini waliambiwa kuwa alihitaji huduma ya dharura katika hospitali kubwa zaidi.

“Tulitoka na mgonjwa kwenye ambulensi na kuelekea hospitali ya Moi saa nane mchana lakini tulipofika katika hospitali hiyo tulishangaa kuwa walikataa kumpokea mgonjwa wetu,” alisema.

Alidai kuwa waliambiwa wasubiri katika ambulensi mpaka hospitali itakapopanga timu ya dharura ya kumpokea.

“Tulisubiri sana lakini hakuna aliyekuja kumhudumia. Tulirudi mara nyingi katika chumba cha huduma za dharura kuomba msaada, lakini hatukupata msaada wowote,” Bi Wakesho alisema.

Alisema kuwa mpwa wake alikuwa na maumivu na alipata shida kupumua na hali yake ikazidi kudhoofika na akafariki.

Bi Wakesho alidai kuwa walikaa katika ambulensi kwa zaidi ya saa mbili, mpaka saa kumi na moja jioni, ambapo mpwa wake alikata pumzi.

“Tulipiga kelele na kuwaita wahudumu ambao walikuja na kumchukua kujaribu kuokoa maisha yake. La kusikitisha ni kuwa tayari alikuwa amekata roho,” alisema.

Alisema kuwa familia hiyo imevunjika moyo na kughadhabishwa na utepetevu wa hospitali kwa kushindwa kuokoa maisha ya mpwa wake.

“Wanawezaje kumwacha mtu afe bila kumhudumia? Wanawezaje kuwa wazembe na bila na huruma? Wanapaswa kuwasaidia watu. Tunalilia haki. Hakustahili kufa hivyo,” alisema,” akasema.

Marehemu ameacha watoto watatu, wenye umri kati ya miaka 15 na saba, ambao walimtegemea yeye kwa elimu na maisha yao.

“Alikuwa ndiye aliyetunza familia yake. Hili ni pigo kubwa kwa familia,” alisema Bi Wakesho.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Kaunti hiyo, Bw Gifton Mkaya alisema kuwa maafisa watatu wamechukuliwa hatua za kinidhamu huku uchunguzi ukiendelea.

Alisema kuwa hospitali ilijutia tukio hilo na imechukua hatua stahiki kuzuia visa kama hivyo kutokea katika siku zijazo.

“Tunajutia tukio hilo na tunatoa rambirambi zetu kwa familia. Tutajitahidi kutoa huduma bora ya afya kwa wakazi, na ndio maana tumechukua hatua hiyo,” alisema.

Bw Mkaya alikiri makosa hayo, akilaumu kutozingatiwa kwa sera ya kitaifa ya uhamisho wa wagonjwa.

Waziri huyo alisema kulingana na picha za CCTV zilizochukuliwa katika hospitali hiyo, mgonjwa alifika katika hospitali ya Moi saa tisa unusu jioni na kuwekwa hapo kwa dakika 58.

Hata hivyo, alisema kuwa timu ya dharura ya hospitali hiyo ingeweza kujaribu kwa haraka kuokoa maisha ya mgonjwa.

“Tumejadili na kuamua kuwa maafisa hao wachukuliwe hatua za kinidhamu kwani hawakutimiza wajibu wao inavyotakiwa,” alisema.

Tukio hilo linatokea takriban miezi miwili tu baada ya familia kudai kuwa mtoto wao alifariki kutokana na kukosa matibabu katika hospitali hiyo hiyo.

Ili kukazuia visa vya uzembe na huduma duni katika hospitali hiyo, Bw Mkaya alitangaza kuwa wameunda jopo ambalo litafanya ukaguzi na mapendekezo ya kuboresha huduma katika kituo hicho cha afya.

  • Tags

You can share this post!

Vuguvugu la Bunge la Mwananchi lachagua rais mpya

Mume anaishi mjini na miye huku mashambani, nahofia...

T L