• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Gavana Waiguru apambana kumiliki nyumba ya Sh200 milioni  

Gavana Waiguru apambana kumiliki nyumba ya Sh200 milioni  

Na RICHARD MUNGUTI

MZOZO wa umiliki wa nyumba ya Sh200 milioni kati ya Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na wakili Chris Kabiro umechacha huku kampuni iliyostawisha mtaa wa Kihingo Village Kitsuru, Nairobi ikisema haimtambui na inamdai ada ya Sh104 milioni.

Na wakati huo huo Kihingo Village (Waridi Gardens) Limited iliyostawisha mtaa huo wenye majumba 55 ya kifahari imeomba Mahakama Kuu kumwamuru Bi Waiguru awasilishe Sh10 milioni kwa msajili wa korti kusimamia gharama za kesi hiyo endapo itatupiliwa mbali.

Mmoja wa wakurugenzi wa Kihingo Bw Gitahi Gethenji aliwasilisha ushahidi mbele ya Jaji Oscar Angote akidai tangu 2015 mpaka sasa Bi Waiguru hajalipa ada ya nyumba ambayo ni Sh1, 092, 800 kila mwezi.

Sasa yapata miaka minane Bi Waiguru ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la magavana nchini (CoG) hajalipa nyumba.

Wakili Gichuki King’ara anayewakilisha Kihingo katika kesi hiyo amedokeza kwamba kulikuwa na agizo la Jaji Eric Ogolla kupinga kuuzwa kwa nyumba hiyo iliyo na mzozo.

Mnamo Desemba 2013, Jaji Ogolla alikuwa ameamuru Kihingo isiuze nyumba hiyo nambari D1 hadi kesi iliyowasilishwa na wakili Chris Kabiro isikizwe na kuamuliwa.

Bw Kabiro anasema kampuni ya Kihingo ilimpa nyumba hiyo kama malipo yake kutokana na kazi aliyokuwa amefanya.

“Hakukuwa na nyumba ya kuuziwa Bi Waiguru. Nyumba nambari D1 anayodai aliinunua nilikuwa nimepewa,” asema Bw Kabiro katika ushahidi aliowasilisha kortini.

Wakili Titus Koceyo anayemwakilisha Bw Kabiro ameeleza mahakama mkataba wa mauzo wa nyumba hiyo uliofanywa na Bi Waiguru sio halali.

“Kulikuwa na agizo la Jaji Ogolla kuzuia kuuzwa kwa nyumba hiyo nambari D1,” asema Bw Koceyo.

Mahakama inaombwa na Bw Kabiro imfurushe Bi Waiguru kutoka kwa nyumba hiyo.

Kampuni ya Kihingo nayo imeeleza mahakama kwamba “haijui jinsi Bi Waiguru aliingia katika nyumba hiyo na inamdai malipo ya nyumba Sh104, 448, 000.”

Katika kesi aliyowasilisha kortini, Bi Waiguru ameomba mahakama kuu iamuru Kihingo imruhusu akamilishe kulipa nyumba hiyo aliyoanza kununua 2019.

Bi Waiguru alimlipa James Ndung’u Gethenji Sh40 milioni kabla ya kuanza kuishi katika nyumba hiyo.

Bw Gethenji ambaye ni mbunge wa zamani wa Tetu  na nduguye Gitahi amekubaliwa na Jaji Angote kujiunga na kesi hiyo kutoa mwanga kuhusu uuzaji wa nyumba hiyo kwa Bi Waiguru.

Kesi itasikizwa Julai 20, 2023.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mkurugenzi taabani kwa kulaghai Jimi Wanjigi shamba

KWPL yapamba moto mechi za msimu zikikaribia kukamilika

T L