NA DAVID MUCHUI
VURUGU zilizuka Jumapili Septemba 17, 2023 katika kanisa la Gavana wa Meru Kawira Mwangaza wakati wa hafla ya kutoa msaada huku umma ukifunga barabara katika eneo la Makiri, Igembe Kusini.
Haya yalijiri huku uhasama ukizidi kutokota kati ya Gavana na Naibu Gavana wake Isaac Mutuma ambaye amelalamikia mara kwa mara kunyanyaswa na bosi wake.
Bi Mwangaza aliyeandamana na mumewe Murega Baicu katika hafla hiyo iliyofadhiliwa na kanisa lao, Baite Family Fellowship (BFF), alisema ng’ombe aliyekusudiwa kutolewa kama msaada kwa wasiojiweza alichinjwa katika ghasia hizo.
Video inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii iliyotumwa na Bi Mwangaza katika ukurasa wake inaonyesha kundi la vijana wakimchinja ng’ombe barabarani huku wakimlaani Gavana.
Kupitia taarifa kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook, Gavana alisema magodoro kadhaa yaliyotolewa kama msaada yalitumiwa vilevile kuwashia moto.
“Tulikumbwa na ghasia ambapo sehemu ya ufadhili wetu uliharibiwa akiwemo ng’ombe aliyenuiwa kunufaisha familia maskini. Tunakemea vikali tabia hiyo iliyopitwa na wakati,” alisema.
“Haifai kuvuruga juhudi za uhisani zinazodhamiriwa kuwasaidia watu wasiojiweza. Tunaamini waliotekeleza vitendo hivyo wanahitaji kukabiliwa kisheria.”
Alitoa wito kwa polisi kuthibitisha alivyoshambuliwa na kuhakikisha haki inatendeka.
“Hata hivyo, tunataka kusisitiza kuwa hatutazuiwa kuendelea na mwito wetu wa kusaidia maskini. Tutaendelea kusaidia wasiobahatika na kuchangia sehemu yetu ya kuboresha maisha ya watu.”
Akijibu kuhusu ghasia hizo, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema polisi wameanzisha uchunguzi na kuwasaka majambazi waliohusika.
“Vurugu za kikatili zinazohusisha wahuni wanaomuunga mkono Gavana na Naibu Gavana wa Kaunti ya Meru mtawalia ni sharti zikome. Uchunguzi utaanzishwa kuhusu waliopanga, kuwezesha na kufadhili ghasia zilizoshuhudiwa katika eneo la Igembe,” alisema.
Waziri alisema hakuna yeyote atanusurika ikiwemo viongozi wa kisiasa katika hadhi zote na vyama vyote vya kisiasa.
Kisa hicho kilitokea siku moja baada ya Mbunge wa Tigania Mashariki Mpuru Aburi kudai kwamba kulikuwa na njama za kuvuruga hafla ya Gavana ya kutoa msaada kwa lengo la kumrushia lawama naibu wake.
Joto la kisiasa mjini Meru limekuwa likizidi kupanda tangu Naibu wa Bi Mwangaza kudai anatengwa katika uendeshaji wa serikali ya kaunti.
Katika kisa cha hivi majuzi, Naibu Gavana alisema alikatiwa umeme katika makazi yake rasmi mjini Meru, katika alichotaja kama hatua ya kumhangaisha kimaksudi.
Bw Mutuma vilevile alidai kuwa stakabadhi zake muhimu ziliibiwa alipokuwa akifurushwa kutoka afisi iliyo karibu na afisi ya gavana.
Naibu Gavana alihamishwa katika jengo kuukuu huku uhusiano kati yake na Gavana ukisambaratika.
Gavana Mwangaza amemshutumu naibu wake kwa kufanya kazi na mahasimu wake kisiasa kupinga uongozi wake.
Wiki iliyopita, Naibu Rais Rigathi Gachagua aliahidi kukutana na viongozi hao wawili kusaidia kusuluhisha tofauti zao.
Subscribe our newsletter to stay updated