• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
Hakimu aahirisha kesi ya Maina Njenga akilaumu polisi kukataza wafuasi kuingia kortini

Hakimu aahirisha kesi ya Maina Njenga akilaumu polisi kukataza wafuasi kuingia kortini

Na JOSEPH OPENDA

Kesi ya kiongozi wa zamani wa Mungiki Maina Njenga imeahirishwa hadi Jumatano, Novemba 22, 2023 baada ya kuzongwa na malalamishi ya unyanyasaji wa polisi na kutishiwa kwa wafuasi waliotaka kuingia kortini.

Hakimu Mkuu wa Nakuru Kipkurui Kibellion katika uamuzi wake Jumanne Novemba 21 alisema kwamba amepata polisi na hatia ya kuhangaisha wananchi dhidi ya kuingia kwenye majengo ya mahakama hivyo kukinzana na hitaji la haki kuonekana kutendeka.

Mahakama hiyo imeagiza kwamba wananchi wafuasi wa Bw Njenga kuingia katika majengo ya mahakama Jumatano na kuwekwe vizuizi vya kiusalama vya kupekua wanaoingia ili kutoa nafasi kwa wale ambao hawatafaulu kutoshea mahakamani.

Kesi ya Bw Njenga ambaye ni mwanasiasa wa Azimio, kuhusiana na ushiriki wake kwenye kundi haramu la Mungiki na maovu yaliyotekelezwa katika eneo la Bahati, Nakuru ilianza kwa ati-ati Jumatatu, Novemba 20, 2023.

Bw Njenga aliwekwa kizimbani kujibu mashtaka baada ya jaribio lake kusitisha kesi hiyo ambapo yeye pamoja na wengine 11 wanakabiliwa na mashtaka saba lilipogonga mwamba.

Hakimu Mkuu Kibellion alitupilia mbali ombi lililokuwa limewasilishwa na kikosi cha mawakili cha Bw Njenja, kikiongozwa na Steve Biko, ambaye alishutumu serikali kwa kugeuza baadhi ya washukiwa kuwa mashahidi bila kufuata sheria.

“Baadhi ya ripoti za mashahidi ambazo tumepewa zilirekodiwa na washukiwa,” akasema Bw Biko.

“Uamuzi wa upande wa mashtaka kugeuza washtakiwa kuwa mashahidi dhidi ya Bw Njenga haukufanywa ifaavyo kwa sababu hakukuwa na ombi kama hilo lililowasilishwa kortini likitaka hatua kama hiyo.”

Bw Njenga vilevile alitaka kesi hiyo isitishwe akisema ilifanana na nyingine anayokabiliana nayo katika mahakama ya Makadara, Nairobi.

Hakimu alitupilia mbali ombi lake, akisema alishindwa kuwasilisha ushahidi kuelezea pingamizi zake hivyo basi akazipata hazina mashiko.

Bw Njenga na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba yanayohusiana na ushirika na kundi lililoharamishwa la Mungiki, kushiriki katika uhalifu eneo la Bahati kati ya Mei 11 na 18, 2023.

Kulizuka kizaazaa kesi ilipokuwa inaanza, wakati shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, ambaye ni mama mkwe wa Bw Njenga, alipozirai akipewa kiapo kabla ya kuanza kuulizwa maswali.

Shahidi huyo ambaye ni mama mkongwe aliyetambuliwa kama Hannah, alizirai na kuanguka muda mfupi baada ya kupandishwa kizimbani kutoa ushahidi dhidi ya mkaza mwana wake na kufanya wahudumu wa mahakama kukimbia kumsaidia.

Chanzo cha kuzimia kwake hakikutambuliwa mara moja.

  • Tags

You can share this post!

Ruto alituenjoi kuhusu mapato ya Tsavo, asema Seneta wa...

Nilidanganywa na Kenya Kwanza, alia Waititu akipigwa na...

T L