• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
Hofu bwanyenye mwingine mashuhuri akiuawa

Hofu bwanyenye mwingine mashuhuri akiuawa

Na JOHN NJOROGE

UTATA unaendelea kuzingira kifo cha mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni moja ya maua, Justus Metho Muinde katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru.

Mwili wa Bw Metho ambaye alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya maua ya Molo Green, ulipatikana ukiwa na majeraha mabaya kwenye mikono, kifua na kichwa kikiwa kimekatwa vibaya.

Mmoja wa marafiki zake alipata mwili huo ukiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Hilux yenye nambari ya usajili KCD 459V kando ya barabara ya Molo-Keringet.

Marehemu alikuwa maarufu kutokana na ukwasi wake wa kibiashara katika mji wa Molo na inadaiwa alikuwa pekee yake alipovamiwa na wahalifu. Polisi wanaamini kwamba waliotekeleza mauaji yake walikuwa wamemfuatilia kwa muda.

Aidha, madirisha ya magari yake pia yalikuwa yamevunjwa“Madirisha yalikuwa yamevunjwa na inaonekana walimsimamisha kabla ya kumuua akiwa ameketi kiti cha mbele,” akasema mmoja wa walioshuhudia kisa hicho.

Makachero tayari wameanza kufuatilia vidokezo ambavyo huenda vikawasaidia kubaini kiini cha mauaji hayo.

Kulingana na Kamanda wa kaunti ndogo ya Molo, Bw Samuel Mukuusi, huenda tajiri huyo aliuawa na watu wasiojulikana eneo hilo.

“Mwili wake uligunduliwa na mmoja wa marafiki zake ambaye alikuwa akiendesha gari barabarani kisha akaona gari lake limeegeshwa kando ya barabara. Alipata madirisha yamevunjwa na kupata Muinde akiwa amefariki,” akasema Bw Mukuusi.

Bw Muinde aliwasihi wakazi kuepuka porojo kuhusu mkasa huo na badala yake kuwaachia maafisa wa polisi wafanye uchunguzi

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Watoto wa mitaani wasidhulumiwe kwa jina...

Mudavadi apuuzilia mbali dai la kuwepo juhudi kufufua NASA