• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Idadi ya waliothibitishwa kufariki Shakahola yagonga 235

Idadi ya waliothibitishwa kufariki Shakahola yagonga 235

NA ALEX KALAMA 

MAAFISA wanaoendeleza operesheni ya kufukua makaburi ili kutoa miili ya watu waliozikwa katika hali tatanishi kwenye msitu wa Shakahola wamepata miili minane mnamo Alhamisi.

Kufikia sasa idadi ya watu waliofariki kutokana na imani potovu imefikia 235 huku idadi ya watu waliokolewa ikifikia 89. Hii ni kwa sababu jana Jumatano miili 15 ilifukuliwa na mmoja ukapatikana kichakani na kufanya idadi ya wahanga kufika watu 227.

Katika taarifa yake ya kila siku kwa vyombo vya habari mshirikishi wa Pwani Rhoda Onyancha amesema katika operesheni hiyo ya Alhamisi watu wanne wameokolewa ambapo mmoja kati yao alikuwa katika hali mbaya zaidi.

“Siku ya leo tumefukua miili minane na pia tumewaokoa watu wanne wakiwa hai msituni ambapo mmoja alikuwa katika hali mahututi na wamekimbizwa katika hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi ili kupata matibabu ya dharura,” amesema Bi Onyancha.

Hata hivyo Bi Onyancha amesema idadi ya watu wanaotafuta jamaa zao waliopotea imeongezeka kutoka 611 hadi kufikia 613 hii ikiwa ni baada ya watu wawili zaidi kuripotiwa kupotea.

“Katika oparesheni ya leo hakuna mtu aliyekamatwa pia vilevile shughuli ya kufukua miili itasitishwa kuanzia kesho Ijumaa ili kutoa nafasi kwa maafisa wetu kujitayarisha kwa shughuli ya upasuaji wa maiti itakayoanza Jumatano wiki ijayo,” amesema Bi Onyancha.

Afisa huyo wa utawala amedokeza kuwa operesheni ya kuwatafuta manusura waliosalia katika msitu huo bado inaendelea kila siku hadi pale watakapomaliza kutoa watu walio kwenye msitu huo.

“Japo shughuli ya kufukua miili itasimama kwa muda lakini operesheni ya kuwatafuta manusura waliokwama msituni itaendelea usiku na mchana. Pia idadi ya watu waliokamatwa tangu kuanza kwa operesheni hadi sasa bado imesalia ile ya 31,” amesema Bi Onyancha.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua: Raila apige tu picha na Rais, hakuna kuingia...

Njia ya Gaspo Women kuendea ubingwa KWPL yageuka telezi

T L