• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:18 AM
Itumbi alia kucheleweshwa kwa kesi ya ‘njama ya kumuua Ruto’

Itumbi alia kucheleweshwa kwa kesi ya ‘njama ya kumuua Ruto’

NA RICHARD MUNGUTI

MWANABLOGU aliyeteuliwa kuwa Waziri Msaidizi wa Masuala ya Teknolojia Dennis Itumbi na ambaye alishtakiwa kwa kusambaza barua feki ya  kufichua njama ya kumuua Rais William Ruto alipokuwa Naibu Rais mwaka 2021, amelalama kortini akisema kesi yake inacheleweshwa.

Bw Itumbi anayeshtakiwa pamoja na Samuel Gateri Wanjiru alilalamika upande wa mashtaka hautaki kukamilisha kesi inayowakabili.

Bw Itumbi aliteta baada ya kiongozi wa mashtaka kuomba kesi hiyo iahirishwe.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Susan Shitubi alifahamishwa kwamba faili ya polisi katika kesi hiyo haikuwasilishwa kortini kwa vile afisa mkuu anayechunguza kesi hiyo yuko likizoni.

“Naomba kesi hii iahirishwe kwa vile sijaletewa faili ya kesi hii ya polisi. Afisa aliyechunguza kesi hii yuko mapumzikoni,” kiongozi wa mashtaka alidokeza.

Aliomba kesi hiyo itengewe siku nyingine ya kusikilizwa.

Bi Shitubi alielezwa Itumbi na Gateri walikuwa waanze kujitetea leo Jumatano baada ya kupatikana na kesi ya kujibu.

Lakini wakili wa Bw Itumbi amepinga vikali ombi hilo akisema: “Washtakiwa wako tayari kujitetea. Hakuna sababu za kutosha zilizotolewa na upande wa mashtaka kuwezesha kesi hii kuahirishwa.”

Mahakama iliambiwa ombi la upande wa mashtaka ni mbinu za kuchelewesha kukamilishwa kwa kesi inayomkabili Bw Itumbi.

Licha ya malalamiko na manung’uniko hayo, hakimu ameahirisha kesi hiyo akisema “upande wa mashtaka hauwezi kulazimishwa kuendelea na kesi kama hauko tayari.”

Pia Bi Shitubi amesema ndiyo mara yake ya kwanza kuhusika na kesi hiyo.

“Hii ndiyo mara ya kwanza kesi hii kuletwa mbele yangu. Nahitaji muda nijifahamishe nayo. Itabidi niiahirishe kumpa muda kiongozi wa mashtaka kuletewa faili ya polisi,” Bi Shitubi amesema.

Ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 29, 2023.

Katika kesi hiyo mawaziri na wabunge kadhaa wanatarajiwa kutoa ushahidi kumtetea Bw Itumbi.

  • Tags

You can share this post!

Oburu Oginga na Ombaka wataka Orengo na naibu wake...

Mackenzie na wenzake wasusia mlo wakidai matamshi ya...

T L