• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:30 AM
UJASIRIAMALI: Jukwaa la kuwapa fursa watu wenye uwezo wa kawaida kujiamini, kupata kazi

UJASIRIAMALI: Jukwaa la kuwapa fursa watu wenye uwezo wa kawaida kujiamini, kupata kazi

NA MAGDALENE WANJA

KATIKA masomo yake ya shule ya upili, Bryan Chesoli alitambulika kama mwanafunzi wa kiwango cha kawaida tu.

Jambo hili lilimfanya ahisi kama kwamba hatoshi mboga kwa kila jambo analolifanya.

Kwa kuhisi hivi, Chesoli alikuwa na hofu sana na aliogopa hata kwenda kwa mahojiano ya kazi kwani gredi zake hazikuvutia.

“Sikuwa mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri darasani na hapo nilipojiunga na chuo kikuu mnamo mwaka 2012, nilifanya uamuzi wa kutafuta ubora wangu,” anaambia safu hii.

Alijiunga na shirika la International Association of Students in Economics and Business (AIESEC), ambalo lilimsaidia pakubwa akaanza kujuana na watu wengi zaidi waliokuwa na maono sawa na yake.

Bryan Chesoli aliunda jukwaa la kipekee kuwapa fursa watu wenye uwezo wa kawaida tu. PICHA | MAGDALENE WANJA

Shirika hilo lilimpa nafasi ya kufanya kazi ya kujitolea katika mitaa ya mabanda.

Alipokuwa katika kazi hio katika eneo la Mukuru, aliweza kukabiliana na janga ukosefu wa ajira kwa vijana.

“Changamoto hii ilinipa nafasi ya kuanzisha mradi wa kuwaunganisha vijana wafanyibiashara ambao walikuwa na uzoefu, ili kuwwafunza jinsi ya kufanya biashara na kujitegemea,” akasema Chesoli.

Katika mwaka wa 2014, alipokuwa na umri wa miaka 19, alianzisha shirika aliloliita Youth Lite, na lengo lake lilikuwa ni kukabiliana na kero ya ukosefu wa ajira.

Bryan Chesoli aliunda jukwaa la kipekee kuwapa fursa watu wenye uwezo wa kawaida tu. PICHA | MAGDALENE WANJA

Kwa sababu ya kukosa mtaji katika siku za awali, Chesoli aliandaa mikutano na wanafunzi katika kanisa la Nairobi Baptist Church.

“Tulipokuwa tukianza, watu wengi walidhani kuwa tulikuwa tukiwapa wanafunzi mafunzo kazini (internship), ila nia yetu ilikuwa ni kuwapa wanafunzi nafasi na fursa ya kubadilishana mawazo na waajiri katika sekta mbali mbali,” anaongeza.

Wanafunzi ambao katika mazingira ya kawaida hawawezi kuonyesha uwezo na ushindani wao katika sekta mbalimbali kutokana na changamoto mbalimbali, hupewa nafasi ya kuajiriwa na kampuni ambazo hupewa nafasi kuwachagua.

Wanafunzi ambao wamejiunga na shirika hili hulipa Sh200 kila mwaka.

  • Tags

You can share this post!

Wasiwasi watoto wakikosa basari za mamilioni ya pesa

TALANTA: Gwiji wa sataranji

T L