• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Kalonzo, Raila kufufua NASA

Kalonzo, Raila kufufua NASA

Na PIUS MAUNDU na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka wametangaza kuwa wataungana ili kumshinda Naibu wa Rais William Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Uhusiano kati ya Bw Odinga na vinara wengine wa muungano wa NASA wanaojumuisha Bw Musyoka, kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula, uliharibika baada ya kiongozi wa ODM kufanya mazungumzo kisiri na kutangaza kushirikiana na Rais Kenyatta mnamo Machi 2018 bila kuwajulisha wenzake.

Jana, viongozi hao walisema kibarua chao cha kwanza kitakuwa kupambana na ufisadi endapo watachaguliwa kuunda serikali mwaka ujao. “Jana (Alhamisi) walisoma makadirio ya bajeti ya Sh3.03 trilioni lakini kiasi kikubwa cha fedha hizo kitaibwa na kuishia kwenye mifuko ya wachache.

“Sisi tunataka kutoa wezi 2022 na kuziba mianya yote ya wizi. Si mliona (hayati) John pombe Magufuli alipoongoza Tanzania kwa miaka mitano tu na alifanikiwa kuangamiza ufisadi? Tutafanya hivyo,” akasema Bw Odinga.

Alikuwa akizungumza katika mazishi ya mbunge wa zamani wa Kibwezi, Kalembe Ndile kijijini Kivuthini, Kibwezi Mashariki, Kaunti ya Makueni.Bw Odinga na Bw Musyoka walipokelewa kishujaa na wakazi wa Kibwezi walipowasili katika mazishi ya Ndile aliyefariki Mei 30, mwaka huu.

Bw Musyoka ni mmoja wa vigogo wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) unaojumuisha Bw Mudavadi, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi na Seneta wa Bungoma Wetang’ula.Bw Odinga, hata hivyo, amekataa kujihusisha na muungano wa OKA – msimamo ambao umefanya wadadisi wa kisiasa kuhisi kuwa huenda akajiunga na Dkt Ruto.

Bw Musyoka na Bw Mudavadi wamekuwa wakimtaka Bw Odinga kuonyesha hisani kwa kuunga mkono mmoja wao katika kinyang’anyiro cha urais 2022.Lakini waziri mkuu huyo wa zamani ameshikilia kuwa hataunga mkono mgombea yeyote wa urais mwaka ujao.

Kauli ya jana inaashiria kuwa Bw Odinga huenda akajibwaga ulingoni tena 2022. Bw Odinga na Bw Musyoka walitangaza kushirikiana 2022 baada ya kuonywa na Gavana wa Kitui, Charity Ngilu kuwa huenda Dkt Ruto akapenya na kushinda urais mwaka ujao iwapo watatengana.

Bi Ngilu ambaye alikuwa wa kwanza kuzungumza alijitolea kuongoza mazungumzo baina ya Bw Odinga na Bw Musyoka ili kuhakikisha wanaungana kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.“Msipoungana mtapoteza 2022 na mimi sitaki kwenda kwa wilibaro,” Bi Ngilu alisema huku akimrejelea Dkt Ruto anayehusishwa na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachotumia nembo ya Wilibaro.

Jana, Bw Musyoka alifichua kuwa uhusiano baina yake na Bw Odinga ungali imara. “Mimi na Bw Odinga tumehangaika pamoja kwa zaidi ya miaka 10 na tutandelea kushirikiana. Muungano wetu wa NASA ungali thabiti. Wakati huo huo,

Bw Odinga alimshambulia aliyekuwa Jaji Mkuu Mutunga aliyemtaka Rais Kenyatta kujiuzulu kwa kukiuka Katiba.Bw Odinga alimtaja Dkt Mutunga kama ‘mnafiki aliyekataa ushahidi wetu katika kesi tuliyowasilisha katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya urais 2013 ambapo Rais Kenyatta aliibuka mshindi.

“Jaji Mutunga alikataa ushahidi wetu kwa kudai kuwa tulichelewa, hiyo si haki. Lakini leo anajitokeza na kudai kwamba Rais amekiuka sheria. Huo ni unafiki mkubwa,” akasema.

Majaji wakuu wastaafu, Dkt Mutunga na David Maraga, mapema wiki hii, walijitokeza na kuwataka wabunge kumtimua Rais Kenyatta kwa kukataa kuwateua majaji sita kati ya 41 waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kutokana na madai kwamba maadili yao yalikuwa ya kutiliwa shaka.

Bw Odinga pia aliwashambulia viongozi wa kidini ambao wanataka mchakato wa kurekebisha Katiba, kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kusitishwa hadi baada ya uchaguzi. “Viongozi wa kidini washughulikie masuala ya kanisa na waachie wanasiasa mambo ya BBI,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Chepng’etich aweka rekodi mpya ya Kenya ya mita 1,500...

Kenya yakopa Sh80b baada kutangaza bajeti ya madeni