• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
KEMSA: Murathe apanga kujitetea mbele ya kamati

KEMSA: Murathe apanga kujitetea mbele ya kamati

Na BENSON MATHEKA

BAADA ya kushutumiwa vikali kwa kuhusishwa na sakata ya mamilioni ya pesa katika Mamlaka ya kusambaza dawa nchini (KEMSA), naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe, amesema kwamba atafika mbele ya kamati ya bunge inayochunguza kashfa hiyo kujitakasa.

Kamati ya Uhasibu ya Bunge (PIC) imemhusisha Bw Murathe na kampuni ya Kilig limited iliyokabidhiwa tenda ya Sh4 bilioni kuuza vifaa vya kujikinga (PPE) kwa Kemsa mwaka 2020.

Bw Murathe ambaye ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta amekanusha kuhusika na kampuni hiyo moja kwa moja.

Baada ya kamati kumhusisha na kampuni hiyo, washirika wa Naibu Rais William Ruto walimshambulia vikali hasa baada ya kuwasilisha hati ya kiapo kwa kamati badala ya kufika binafsi kuhojiwa.

Maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Susan Kihika ( Nakuru) na Aaron Cheruiyot (Kericho), walidai kwamba Bw Murathe hakuwa peke yake katika kampuni hiyo.

“Kinachosikitisha ni kwamba Murathe ni ajenti tu. Kinara ni nani?” alihoji Bw Murkomen.

Akiandika kwenye Twitter, Seneta maalum, Bi Millicent Omanga, alisema Murathe hawezi akaguswa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, ambaye pia ni mbunge wa Mvita, Bw Abulswamad Nassir, alisema jana kuwa kamati hiyo imemwalika tena kufika Alhamisi ijayo baada ya kukosa kufika Alhamisi iliyopita.

Bw Murathe anatarajiwa wiki ijayo kufafanua masuala aliyotaja katika hati yake ya kiapo.

Kulingana na gazeti la Business Daily, Bw Murathe anafaa kufika mbele ya kamati hiyo Alhamisi.

Mnamo Ijumaa alinukuliwa akisema kwamba atafika kutakasa jina lake akisisitiza kwamba hakunufaika na tenda yoyote inavyodaiwa.

Kwenye hati yake ya kiapo kwa PIC, Mbunge huyo wa zamani wa Gatanga anasema kwamba alikuwa mdhamini wa kampuni ya Kilig na sio mkurugenzi au mmiliki wake.

Aliapa kufika mbele ya kamati Alhamisi ijayo “kumwaga mtama” akisisitiza kwamba yeye sio mmiliki wa kampuni hiyo na hakunufaika na mabilioni ya sakata ya Kemsa.

  • Tags

You can share this post!

Maiti ya ajuza aliyefariki 2004 hatimaye yazikwa

NASAHA ZA RAMADHAN: Sasa ni wakati bora wa kuzidisha...