NA BRIAN AMBANI
KAMPUNI ya Kenya Power imeanza mikakati ya kubinafsisha baadhi ya shughuli zake za kusambaza umeme nchini.
Tayari, kampuni hiyo imetoa tangazo ikiwarai wawekezaji wa kibinafsi ambao wangetaka kuchukua baadhi ya shughuli za kusambaza umeme kuwasilisha nia zao kwake.
Wawekezaji hao wamepewa hadi Oktoba 18, kuonyesha nia ya kusambaza umeme katika baadhi ya mitaa tisa ya mabanda jijini Nairobi.
Mitaa hiyo haijaunganishwa kwenye laini ya kitaifa ya kusambaza umeme.
Mnamo Ijumaa, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Dkt Joseph Siror, alieleza sababu ya hatua hiyo mpya.
“Kile tumebaini ni kwamba kuna maeneo ambayo hayajaunganishwa na mfumo wa kusambaza umeme huku mengine yakiwa yameunganishwa vibaya. Kutokana na hali hiyo, tulijiuliza kuhusu njia tunayoweza kutumia kuhakikisha watu hao wamepata huduma za umeme vizuri. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mpango huo,” akasema Dkt Siror kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Baadhi ya mitaa iliyopangiwa kuwekwa kwenye mpango huo ni Mukuru, Mathare, Kibera, Kibagare, Deep Sea, Mji wa Huruma, Githogoro, Kiambiu na Kamukunji.
Wawekezaji wanatarajiwa kutengeneza na kudumisha mfumo wa kusambaza umeme wa viwango vya juu na chini, kuweka mitambo ya kupima kiwango cha umeme alichotumia mteja na kukusanya ada za matumizi ya umeme kutoka kwa watumizi.
Subscribe our newsletter to stay updated