• Nairobi
  • Last Updated December 3rd, 2023 8:00 PM
Kenya yapokea vifaa vya kidijitali kuimarisha uangalizi wa maradhi mipakani

Kenya yapokea vifaa vya kidijitali kuimarisha uangalizi wa maradhi mipakani

NA MARY WANGARI

JUHUDI za kukabiliana na milipuko na majanga ya maradhi mbalimbali yanayoambukizwa kupitia maeneo ya mipaka nchini zimepigwa jeki kufuatia ufadhili wa vifaa vya kidijitali vya kuboresha uangalizi.

Wizara ya Afya jana ilipokea vipakatalishi saba, tarakilishi 37, Vifaa vya Kuhifadhi Umeme (Ups) 37, nyaya za kupitishia umeme 37 na vituo vinne vya kuunganishia intaneti.

Vifaa hivyo vitawekwa katika maeneo mahsusi kwenye vituo muhimu vya mipakani kama vile Busia, Malaba, Mandera na Moyale, alisema Katibu wa Wizara katika Idara ya Afya ya Umma na Viwango vya Kitaaluma, Mary Muthoni.

Aidha, vifaa hivyo vya kidijitali vinadhamiriwa kuboresha mawasiliano na usambazaji wa data baina ya maeneo husika hivyo kuwezesha hatua mwafaka kuhusiana na tishio la kuzuka kwa maradhi.

Ufadhili huu uliofanikishwa kupitia ushirikiano baina ya Muungano wa Uropa, Ujerumani na Wizara ya Ushirikiano Kiuchumi na Maendeleo (BMZ), unatazamiwa kuimarisha pakubwa juhudi za Wizara ya Afya kuanzisha mfumo wa kidijitali kuhusu uangalizi mipakani.

Kwa mujibu wa Bi Muthoni, hatua hii ni sehemu ya “Suluhu za Kidijtali za Umoja wa Uropa katika Kuimarisha Uangalizi kuhusu Maradhi na Mifumo ya Uangalizi kuhusu Covid-19 katika mataifa wanachama wa Mamlaka ya Maendeleo Baina ya Serikali (IGAD).”

“Hii ni hatua muhimu kuhusu ugunduzi na udhibiti wa mapema kuhusu milipuko ya magonjwa,” alisema BiMuthoni.

“Ufadhili kutoka kwa washiriki wetu unaashiria kipindi muhimu katika kuimarisha mifumo yetu ya afya ya umma na kuimarisha ushirikiano baina ya mipaka. Pamoja, tuna uwezo zaidi wa kukabiliana na mikurupuko ya, milipuko na majanga hivyo kuhakikisha Kenya na Upembe wa Afrika ulio salama.”

  • Tags

You can share this post!

Mackenzie kuendelea kufungiwa ndani serikali ikisema...

Wakenya sasa wakimbilia Tanzania kutafuta petroli bei nafuu

T L