• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 4:53 PM
Kilichomng’oa Sheffie Weru kazini chapata shahidi mpya, asema ni upuuzi tu

Kilichomng’oa Sheffie Weru kazini chapata shahidi mpya, asema ni upuuzi tu

Na MWANGI MUIRURI

Kisa cha wapenzi wawili ambacho kimeishia kumng’oa kazini mtangazaji mwenye uzooefu mkubwa Shaffie Weru kutoka ajira ya Radio Africa Group kimechukua mwelekeo mpya baada ya shahidi kujitokeza akidai kiliripotiwa kwa njia isiyotilia maanani ukweli.

Katika kisa hicho, Bi Eunice Wangari anasemwa kuwa alikutana na Bw Moses Gatama katika mtandao wa Facebook na wakaamua kukutana ili wafahamiane zaidi.

Ripoti zinasema kuwa wawili hao walikutana katika nyumba ya Bw Gatama na ambapo kulizuka ufisi fulani kutoka kwa mwanamume huyo wa kutaka kuonja asali siku iyo hiyo, mrembo akikataa.

“Ndipo mvutano ulizuka na ulioishia mrembo huyo kurushwa nje ya gorofa la 12 la nyumba ya mwanamume huyo na ambapo alipata majeraha mabaya na kuishia kukamatwa kwa Bw Gatama,” ripoti hizo zikasema.

Sasa, Bw Paul Mugenda (pichani), akiwa ni Mkurugenzi wa Paris Group of Companies anasema kuwa Bw Gatama ni mwaajiriwa wake.

Bw Mugenda anaelezea kuwa kisa hicho kilitokea katika mojawapo ya afisi zilizoko katikati mwa Jiji la Nairobi.

Anasema kuwa ni kisa cha Jumapili iliyopita masaa ya jioni ambapo vipenzi hao wawili walinunua chakula na mivinyo na wakaamua kuingia afisini kujivinjari.

Anasema kuwa kama mwaajiri wa Bw Gatama, ni sera kuwa afisi hizo hazifai kuwa na wafanyakazi siku ya Jumapili, akilaumu walinzi kwa kukubali ukiukaji dhidi ya sera hiyo utekelezwe.

Anasema kuwa wawili hao walikunywa na wakalewa vibaya na ndipo kukazuka kisa kilichoishia Gatama kukamatwa na maafisa wa polisi wa Central, Nairobi.

Bw Mugenda anasema kitu cha kwanza alifanya baada ya kupokea habari hizo ni kumfuta kazi Bw Gatama kwa kukiuka sera za kampuni.

Bw Mugenda anasema kuwa Bw Gatama na Bi Wangari ni wapenzi wanaofahamiana vyema na kisa hicho chote ni cha kifamilia.

Bw Mugenda anasema kuwa wawili hao baada ya kulewa walianza kubishana na ndipo mwanamke huyo aliruka kutoka gorofa la 12 na akaangukia paa la gorofa la Tisa—hali ambayo pia inazua maswali kuhusu urefu huo na unusurike ukiwa mwanamke na ambaye ni mlevi, ikizingatiwa kuwa nyumba za gorofa hazijaezekwa kwa mabati au magondoro bali paa ni sawa na baranbara ya lami!

Katika hali hiyo, Bw Mugenda anashauri wanaoandika kuhusu suala hili wajiepushe na ukora wa kimawazo na ambao unapindua hali na kugeuza kisa kama hichi kuwa cha kushambulia wanaume kuwa ni wanyama.

“Wanaoandika hata hawajui kisa kilifanyika wapi na hakuna aliyekuwa ndani ya usiri huo wa wawili hao ndani ya afisi yangu ndio ajue mrembo alirushwa na hatimaye mbona hakuna nukuu za taarifa ya mlalamishi,” asema.

Ni habari hizo ambazo zilichambuliwa na Bw Shaffie na akaishia kufutwa kazi.

Shaffie akiwa na wenzake Studioni Neville Muasya na DJ Mfalme walianza kuchambua kisa hicho na ikawa moto.

Shaffie alisisitiza msimamo wake kwamba ikiwa wanawake wanataka kupata afueni ndani ya dunia ya mafisi, ni lazima wajiwekee vigezo vya kutangamana na kukumbatia uchumba.

Alisema kuwa ni lazima wanawake wajiangazie kama wasiopatikana kwa urahisi na ikiwa ni lazima wakutane kabla ya kuzoeana, iwe ni katika maeneo yasiyo pembeni na usiri hatari.

Hapo ndipo wasimamizi wa mitambo ya Homeboyz Radio baada ya Shaffie kukemewa katika mitandao ya kijamii waliamua kuwafuta wote watatu kazi.

Hii ilikuwa ni baada ya serikali kutoza kituo hicho faini ya Shilingi Moja Milioni na kupiga marufuku Shoo ya Shaffie ya Lift-Off kwa kipindi cha nusu mwaka na ikamwamrisha mtangazaji huyo aombe msamaha kwa mitambo na pia kwa vyombo vya habari.

Tayari Shaffie ako mahakamani akisaka fidia ya Sh21 Milioni kwa madai ya kufutwa kazi kwa njia haramu ambapo anadai alitumiwa ujumbe wa WhatsApp mwendo was aa 11 usiku hivyo basi kukosa urasmi unaofaa kuzingatiwa.

Kisa chote kikiangazia jinsi kutegemea habari zisizotimiza vigezo vya uadilifu wa maandalizi, ukosefu wa uchunguzi wa kina na wakubwa serikalini na katika makampuni ya kibinafsi kukimbia kutekeleza adhabu ili kujipa umaarufu…huishia kuvuruga kila safu ya mkondo wa haki.

[email protected]

You can share this post!

SHAIRI: Korona kufuli nzito

Hesabu za Uhuru 2022 zamkosesha usingizi