Na MUSSA JUMA, Mwananchi Communications Limited
Naibu Mwenyekiti wa chama cha Upinzani Chadema, Tundu Lissu na viongozi wengine wa chama hicho waliokuwa wamekamatwa wilayani Karatu, Arusha wamepewa dhamana na kuachiliwa baada ya kuandikisha taarifa katika kituo kikuuu cha polisi Arusha.
Viongozi hao walikuwa wanatuhumiwa kufanya mikusanyiko bila kuwa na kibali na kufunga barabara ya Karatu kuelekea Nyorongoro huku Lissu akiwasifu polisi kwa ustaarabu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu Septemba 11, 2023, baada ya kuandikisha taarifa, Lissu ambaye alikuwa na kaka yake Wakili Alute Mughwai alisema baada ya kuandikisha taarifa, aliambiwa kurejea baada ya mwezi mmoja.
Lissu anasema tuhuma ambazo zilikuwa akihojiwa zilikuwa kuhusu kufanya mkusanyiko usio halali na kufunga barabara.
“Nimewaeleza mimi sijafanya mkusanyiko na sikufunga barabara kwani waliofunga ni polisi wakati wanatuzuia kuendelea na safari kwenda Ngorongoro,” akasema.
Akaelezea kwamba baada ya polisi kufunga barabara na kuona wanataka kupiga watu ndipo waliamua kukaa barabarani na hawakufunga barabara.
Hata hivyo, amesema safari hii Jeshi la Polisi tangu lilipowakamata halikuwafanyia kitu kibaya badala yake liliwahoji ‘kistaarabu’.
“Hii sio mara yangu ya kwanza kukamatwa, safari hii sikulala ndani tangu waliponikamata hadi saa hizi hawajanifanyia chochote ambacho naweza kusema sio kizuri, polisi wamekuwa wastaarabu sana tangu waliponikamata Jumapili,” akasema.
Hata hivyo, anasema kukamatwa kwake na viongozi wengine hakutawazuia kurejea kufanya mikutano Ngorongoro na Karatu.
“Tunakwenda kujipanga kwa ajili ya mikutano ya kanda ya kaskazini, tutakwenda Ngorongoro kwani sio gereza na tutakwenda Karatu,” akasema.
Lissu alirejea Tanzania kutoka Ubelgiji, baada ya Rais Samia kuondoa marufuku ya kuandaa mikutano ya kisiasa iliyokuwa imedumu kwa miaka sita.
Alikuwa akiishi Ubelgiji tangu 2020, alikotorokea baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa urais na marehemu John Magufuli.
Mnamo Jumapili, polisi walisema kuwa Lissu na watu wengine watatu walizuiliwa ili kuhojiwa, baada ya kushtakiwa kwamba walikuwa wakifanya mikutano iliyo kinyume cha sheria na kuwazuia polisi kufanya kazi yao.
Kwenye video fupi iliyowekwa kwenye mtandao wa X, Lissu alionekana pamoja na wanachama wengine wa chama hicho wakionyesha alama ya ‘V’, kuashiria ushindi.
Alama hiyo huwa inatumiwa na CHADEMA kwenye mikutano yake ya kisiasa.