• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
KRA yaelekeza mkono wake kwa mabilioni ya mawakili kwenye tangazo jipya

KRA yaelekeza mkono wake kwa mabilioni ya mawakili kwenye tangazo jipya

Na RICHARD MUNGUTI

MAMLAKA ya Ushuru nchini (KRA) inalenga kampuni za mawakili nchini katika jitihada zake za kutoza ushuru mabilioni ya pesa za wateja zinazohifadhiwa katika hazina maalum za wanasheria.

Hatua hii ya KRA imesababisha mtafaruku mkuu katika kampuni za mawakili ambazo zimepinga vikali mpango huo wa KRA zikisema inakiuka haki za wateja wao.

Hatua hii ya KRA kuelekeza mkono wake kwa kampuni za mawakili inatokana na agizo la Rais William Ruto na Wizara ya Fedha kuwa ifanye juu chini hadi ikusanye ushuru wa takriban Sh2.57 trilioni.

Chama cha mawakili nchini (LSK) kimepinga vikali hatua hiyo kikisema inalenga kukiuka haki za wateja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoonwa na Taifa Leo, KRA imeiandikia barua kampuni moja ya mawakili ikitaka ilipe ushuru wa mteja wake tangu 2018.

Katika arifa kwa kampuni hiyo ya mawakili, KRA imetaka ushuru wa thamani ya mapato (VAT) kuanzia 2018.

Kulingana na ushahidi uliopo, kampuni hiyo ya mawakili imesisitiza kuwa imekuwa ikilipa ushuru huo wa VAT na kulingana na ushahidi haidaiwi chochote na KRA.

“Tunaendelea na harakati ya kuthibitisha malipo ya ushuru wa VAT wa kampuni yako ya mawakili kati ya Januari 2018 hadi leo,” KRA ilisema katika barua iliyotumwa kwa kampuni hiyo ya mawakili mnamo Septemba 2023.

Katika waraka huo, KRA inaitaka kampuni hiyo ya mawakili iikabidhi ushahidi wa ununuzi bidhaa,taarifa za benki na risiti za kila mwezi za kieletroniki.

“Tunashauri kwamba uchunguzi tunaofanya utashirikisha tu mauzo, ununuzi na risiti za kieletroniki,” idara ya ushuru wa ndani ya KRA ilieleza katika barua hiyo.

Huku KRA ikishuku kuwa kampuni nyingi za mawakili zimekuwa zukikwepa kulipa ushuru, LSK imeseka mamlaka hiyo inajaribu kupata ushuru kwa njia isiyo halali kutoka kwa wanachama wake.

Rais wa LSK, Erick Theuri alisema kampuni za mawakili huweka rekodi mara mbili.

Rekodi moja ni ya afisi ya kampuni husika na ile nyingine hupewa mteja.

Bw Theuri alisema mawakili huwekeza pesa hizo za wateja katika akaunti zinazozaa faida.

Faida inayotokana na uwekezaji huo hupewa mteja husika.

“Kile kinachoendelea kufanyika sasa ni KRA kukagua akaunti za wateja kubaini kiwango cha pesa ambacho kila wakili amewekeza kwa niaba ya mteja muhusika.Pia inamulika faida iliyopatikana kutokana na pesa hizo,”Bw Theuri alisema.

Kinara huyo wa LSK alisema kuwa KRA hufanya hesabu ya faida iliyopatikana kisha inatoza asilimia 15 ya faida hiyo kama ushuru.

KRA huhesabu faida hii kama mapato ya kampuni hiyo ya mawakili.

Lakini mawakili wamesema hawabaki na pesa zozote kwa kuwa wanawapa wateja pesa hizo za faida. LSK imewataka wanachama wake wanaozidi 20,000 wawasilishe malalamiko endapo wanahisi KRA inawasumbua kwa kudaiwa walipe ushuru kutokana na pesa za wateja.

“Baraza la LSK linasikitishwa na idadi kubwa ya malalamiko kutoka kwa wanachama wake kuhusu masumbufu ya KRA ikidai kodi kutokana na pesa za wateja,” alisema Florence Muturi, afisa mkuu wa LSK.

  • Tags

You can share this post!

Majina ya watoto 131 walioangamia Shakahola yajulikana kesi...

Pwani yazama El Nino ikitishia kunyima hoteli mahanjam ya...

T L