• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
LAMU: Gavana Twaha ajiteua kuhudumu kama waziri

LAMU: Gavana Twaha ajiteua kuhudumu kama waziri

NA KALUME KAZUNGU

GAVANA wa Lamu, Fahim Twaha amefanya mabadiliko makubwa kwenye baraza lake la mawaziri huku akijitengea nafasi mojawapo ya uwaziri kwenye baraza hilo jipya.

Kwenye mabadiliko hayo yaliyotangazwa rasmi na katibu wa kaunti, John Mburu, Bw Twaha sasa amejiteua kuwa Waziri wa Afya ya Umma, Mazingira, Miundomsingi ya Maji-taka na Manispaa ya Lamu.

Bw Twaha pia alimteua Naibu wake, Abdulhakim Aboud Bwana kuwa Waziri wa Masuala ya Usalama wa Chakula, Maendeleo ya Viwanda, Uvuvi na Maji.

Mabadiliko hayo yalishuhudia uteuzi wa sura mpya, ambapo Josephat Musembi Matei alichaguliwa kuwa Waziri wa Biashara, Utalii na Viwanda, nafasi ambayo ilikuwa imeachwa wazi tangu 2019 baada ya aliyeshikilia wadhfa huo, Dismas Mwasambu Pole kujiuzulu.

Twaha pia aliwahamisha mawaziri kadhaa kutoka kwa nyadhfa zao za zamani hadi kwenye nafasi tofauti.

Miongoni mwa walioathiriwa ni Waziri wa Ardhi na Mipango, Fahima Araphat ambaye alihamishiwa Wizara ya Fedha, Masuala ya Bajeti and Mipango ya Kiuchumi ilhali Waziri Ahmed Hemed akihamishiwa Wizara ya Ardhi na Mipango kutoka kwa Wizara ya Fedha na Mipangilio ya Kiuchumi.

Aliyekuwa Waziri wa Afya ya Umma na Maji, Abdu Godana Dae alihamishiuwa kwenye Wizara ya Masuala ya Huduma na Utendakazi wa Umma na Utawala.

Mawaziri ambao nafasi zao hazikuguswa na Paul Thairu ambaye ataendelea kushikilia wadhfa wake wa kuwa Waziri wa Elimu, Huduma za Vijana, Jinsia, Michezo na Jamii na Anne Gathoni ambaye ataendelea kuhudumu kama Waziri wa Masuala ya Matibabu.

Akihutubia umma wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri hao, Bw Twaha alisema alichukua hatua ya kutekeleza mageuzi hayo ili kuboresha utendakazi wa serikali yake.

Gavana Twaha aliwahimiza waliochaguliwa kufanya kazi kwa bidii ili wananchi wa Lamu wafaidike na utendakazi wao.

Pia aliwaonya dhidi ya kujihusisha na ufisadi.

“Tumefanya mabadiliko haya dhamira kuu ikiwa ni kuboresha utendakazi na utoaji wa huduma kwa wananchi wetu. Mjitolee kufanya kazi kwa bidi ili Lamu isonge mbele kimaendeleo,” akasema Bw Twaha.

You can share this post!

Mbio za Nyika za Pwani kufanyika Wundanyi Jumamosi

Django FC inavyokuza talanta za chipukizi wa Uthiru