• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
LEONARD ONYANGO: Siku ya Utamaduni ilifaa kuadhimishwa kipekee

LEONARD ONYANGO: Siku ya Utamaduni ilifaa kuadhimishwa kipekee

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya serikali kutangaza Oktoba 10 kuwa Siku ya Utamaduni bila kuandaa maadhimisho ya kitaifa, ni kazi bure.

Waziri wa Masuala ya Ndani, Dkt Fred Matiang’i alipotangaza, wiki iliyopita, kwamba leo ni siku ya mapumziko kufidia Oktoba 10 ambayo ilifanyika jana, aliwataka Wakenya kusherekea Siku ya Utamaduni kwa njia inayodumisha umoja na utangamano wa kitaifa.

Serikali ilistahili kuwa kielelezo kwa kuandaa maonyesho makubwa ya kitaifa ya siku mbili ambapo wawakilishi kutoka jamii zote nchini wangekutana.

Maonyesho sawa na hayo pia yalifaa kufanyika katika kaunti zote 47 ili kutoa fursa kwa jamii mbalimbali mila, desturi na historia yao.

Sherehe za Utamaduni zilifaa kusherehekewa kwa siku mbili kwa sababu hii ni mara ya kwanza kwa siku hiyo kuadhimishwa humu nchini.

Huku Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 ukikaribia, Wakenya walifaa kutumia siku ya jana kujielimisha kuhusu utamaduni wa jamii nyingine.

Ufahamu kuhusu mila na desturi za jamii nyingine ni njia mojawapo ya kuleta utangamano nchini.Uhasama wa kikabila unaoshuhudiwa humu nchini unatokana na watu kutoelewa vyema jamii nyingine.

Rais Kenyatta ambaye amekuwa akikariri kwamba analenga kuacha Wakenya wameungana baada ya kustaafu mwaka ujao, angetumia maonyesho hayo kuhubiri umoja na mshikamano nchini.

Mnamo 2019, Baraza la Mawaziri liliidhinisha Oktoba 10 kuwa Siku ya Utumishi na ‘Boxing Dei’ – ambayo husherekewa Desemba 26 baada ya Krismasi – kuwa Utamaduni.

Rais Kenya aliwataka Wakenya kusherekea Boxing Dei kwa kuzingatia mila za Kiafrika badala ya kufuata desturi za kigeni bila kujua maana.

Lakini inaonekana serikali imebadili na sasa Siku ya Utamaduni itakuwa ikiadhimishwa Oktoba 10 na Desemba 26 itakuwa Huduma Dei.

Tangu 1988, Wakenya walikuwa wakiadhimisha Siku ya Moi kila Oktoba 10 hadi 2010 ambapo jina hilo lilifutiliwa mbali na Katiba mpya.

Kati ya 2010 na 2017, siku hiyo haikuwa ikisherekewa hadi pale Jaji George Odunga aliposema kuwa Oktoba 10 ingali sikukuu ya kitaifa kwa mujibu wa Katiba na akaagiza serikali kuhakikisha kuwa inaadhimishwa.Kati ya 2018 na 2020, siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa lakini bila kitu cha kusherekea.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), nusu ya lugha 7,000 zinazozungumzwa kote duniani, zitakufa kufikia mwishoni mwa karne hii ya 21.

Utamaduni na lugha kadhaa zinazozungumzwa na jamii mbalimbali ni miongoni mwa zitakazotoweka.Siku ya Utamaduni iwapo itaandaliwa vyema, itatoa fursa kwa watoto kujifahamisha mengi kuhusiana na utamaduni wa jamii za humu nchini kabla ya kutoweka.Hivyo, serikali haina budi kuichukulia kwa uzito Siku ya Utamaduni itakapoadhimishwa tena mwaka ujao.

You can share this post!

Mipasuko UDA na Jubilee yaibua vyama vipya Mlimani

Radol alenga kutinga anga za kimataifa katika uigizaji

adminleo