• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Mabilioni yasubiri watu binafsi serikali ikifungua milango ya usimamizi wa bandari

Mabilioni yasubiri watu binafsi serikali ikifungua milango ya usimamizi wa bandari

NA ANTHONY KITIMO

KAMPUNI za kibinafsi zitaanza kufaidika na mabilioni ya pesa za usimamizi wa bandari nchini, baada ya serikali ya kitaifa kutangaza nia ya kubinafsisha baadhi ya gati kwenye bandari ya Mombasa na Lamu.

Tangazo hilo ni dhahiri kuwa serikali ya Rais William Ruto imebadili msimamo baada ya kupinga hatua ya serikali iliyopita kupeana usimamizi wa bandari hizo kwa kampuni binafsi.

Katika tangazo Jumatatu Septemba 11, 2023, Mamlaka ya Kusimamia Bandari za Kenya (KPA) inanuia kushirikiana na kampuni za kibinafsi kuendesha gati tatu za Lamu, nne Mombasa na sehemu maalumu ya zamani ya kuwekea makasha.

Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Bw William Ruto, aliomba kampuni kutuma maombi yao kabla Oktoba 12 ili kuorodheshwa kwa kampuni zitakazomiliki sehemu hizo.

“KPA inaomba kampuni zilizohitimu kutuma maombi kabla Oktoba 12 mwaka huu ili kupewa fursa ya kusimamia gati (1-4) katika bandari ya Mombasa na bandari mpya ya Lamu yenye gati tatu,” alisema Bw Ruto.

Rais Ruto na Kenya Kwanza walikuwa mstari wa mbele kupinga pendekezo la serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kubinafsisha usimamizi wa bandari ya Mombasa, habari hizo zilipochipuka.

Hata hivyo, sasa serikali yake imeonekana kulegeza msimamo na iko mbioni kutekeleza sheria iliyopitishwa mwaka 2019 iliyompa Waziri wa Fedha mamlaka ya kuhusisha kampuni za kibinafsi kuendesha bandari za humu nchini.

Hata hivyo, tangazo la jana limezua maoni tofauti miongoni mwa wadau: wengine wanahofia kupoteza kazi huku baadhi wakiachwa na maswali jinsi serikali iliafikia kubinafsisha shirika ambalo limekuwa likipata faida ya zaidi ya bilioni 15 kila mwaka.

“Kwa sasa serikali ingeweka mikakati ya kuongeza faida kwani kubinafsisha bandari kutafaidi tu kampuni za kibinafsi,” alisema Bw Nasseb Mbarak, mmoja wa wadau bandarini.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Chama cha Kimataifa cha Wasafirishaji na Wenye Mabohari (KIFWA), Bw Roy Mwanthi, aliunga mkono kampuni ya kibinafsi kuendesha bandari ya Lamu.

“Bandari ya Lamu inahitaji hilo ili kuiboresha kwani tangu ifunguliwe rasmi mwaka 2021 ni meli 22 pekee zimetia nanga. Hatuna budi kuhusisha kampuni za kibbinafsi ilimradi hatua italeta mapato zaidi,” alihoji Bw Mwanthi.

Awali, viongozi wa kisiasa eneo la Pwani walikuwa wakipinga kubinafsishwa kwa bandari nchini wakisema kuwa, haiwezekani serikali itumie mabilioni kujenga miundomsingi katika bandari kisha ipokeze shirika la kibinafsi kuisimamia.

Mwezi wa Julai, Rais Ruto aliahidi kuimarisha biashara katika bandari ya Lamu na kupanua ile ya Mombasa kwa lengo la kuongeza mapato.

Baadhi ya sehemu za bandari mjini Mombasa zimekuwa kwa mikono ya kampuni za kibinafsi lakini baadhi ya mikataba hiyo imekuwa siri huku kampuni hizo zikisemekana kufaidi pakubwa kutokana na mipango hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Kiongozi wa Upinzani Tanzania Tundu Lissu ashukuru polisi...

Nanjala kupiga jeki maandalizi ya Harambee Starlets gozi la...

T L