• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:13 PM
Mafisadi katika utoaji wa chanjo waonywa

Mafisadi katika utoaji wa chanjo waonywa

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imetoa onyo kali kwa wahudumu wa afya wanaosakata ufisadi katika utoaji wa chanjo ya virusi vya corona.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya, Dkt Mercy Mwangangi Jumatano alisema wizara imepokea malalamishi kuhusu wahudumu wa afya wanaoitisha hongo ili kutoa chanjo.

Dkt Mwangangi alionya watakaopatikana na hatia kuhusika wataadhibiwa kisheria. Waziri alisema leseni zao zitafuliwa mbali, na kushtakiwa.

“Tumepokea ripoti baadhi ya vituo na wahudumu wanapokea hongo kuwapa watu chanjo, ili wasipige foleni. Watakaopatikana na hatia kuhusika, tutawachukulia hatua kisheria,” Dkt Mwangangi akatangaza.

“Kwa wahudumu wanaoshiriki kitendo hicho haramu, tutafutilia mbali leseni zenu,” akaonya Waziri.

Kaunti ya Nakuru, baadhi ya wakazi waliojitokeza kupokea chanjo katika vituo mbalimbali wamelalamikia ufisadi kusakatwa na hata kuitishwa hongo.

Dkt Mwangangi alisema chanjo ya AstraZeneca na inayoendelea kutolewa nchini, haina malipo yoyote. “Inapatikana bila malipo katika vituo vyote vya afya; umma na kibinafsi, vilivyoidhinishwa kuisambaza,” akasisitiza.

You can share this post!

‘One Kenya Alliance haitegemei kumuondoa Raila kwa...

SHAIRI: Korona kufuli nzito