• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 AM
Magavana walia serikali yaua ugatuzi

Magavana walia serikali yaua ugatuzi

NA STEVE OTIENO

MAGAVANA sasa wanalia kuwa Serikali ya Kitaifa imeanza kuyachukua majukumu yaliyogatuliwa, kwa kuzinyima kaunti ufadhili wa shughuli hizo.

Walitaja wizara za Afya na Kilimo kuwa zinazoingiliwa, jambo linalorejesha nyuma hatua zilizopigwa miaka kumi iliyopita. Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana Ijumaa, walisema kuingiliwa kwa shughuli za afya na serikali ya kitaifa, kumesababisha maafa na manung’uniko kwa wananchi mashinani.

“Baraza la Magavana (CoG) linaitaka wizara ya Afya ikome kuzichukua huduma za afya pamoja na kuingilia utendakazi wa serikali za kaunti,” alisema mwenyekiti wa CoG, Anne Waiguru.

Taifa Leo pia imepata habari kwamba magavana wanazozana na serikali kuhusiana na mipango ya wizara ya Afya kutaka kuwawezesha watoaji huduma za afya kwa jamii bila kuwashirikisha, ilhali watakuwa wakifanya kazi chini ya serikali za kaunti.

Wakuu hao wa kaunti wanasema hawajafurahishwa na mpango wa wizara ya Afya kutenga Sh519 milioni za kuwalipa wahudumu hao wa afya kwa jamii.

Pia, serikali inawapa simu na vifaa vingine vya kutembea navyo mitaani, ilhali wafanyakazi wanaotoa huduma katika kaunti wamesahauliwa. Barua ya Mei 11 ambayo Taifa Leo iliiona, inaonyesha kuwa wizara ya Afya ilipanga kuanza mpango wa uhamasishaji kutoka Mei 15 hadi Mei 20, kwa watoaji huduma za afya kwa jamii kuhusu jinsi ya kutumia vifaa walivyopewa.

Mpango huo haujawafurahisha magavana, hasa kutokana na kwamba serikali ya kitaifa inatafuta usaidizi kutoka kwa wafadhili, ilhali ni wafadhili hao hao wanaofadhili miradi katika kaunti.

“Tunawasihi washirika katika maendeleo, waache kuunga mkono au kufadhili wizara za serikali ya kitaifa ambazo shughuli zake ziligatuliwa. Mtindo huu unaonekana sana katika wizara za Afya na Kilimo,” alisema Bi Waiguru.

Gavana wa Tharaka Nithi, Muthomi Njuki ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika CoG, alieleza kuwa Katiba iko wazi kuhusu shughuli za afya kugatuliwa.

Aliionya serikali kupitia wizara ya Afya isithubutu kutekeleza majukumu yaliyogatuliwa, kupitia washirika wa kimaendeleo.

“Kaunti zina matatizo mengi katika utekelezaji wa shughuli zilizogatuliwa. Hospitali hazina madawa. Tunataka uchunguzi kuhusu Shirika la Kusambaza Madawa (Kemsa) ufanywe kwa kina na haraka,” akasema Bw Njuki.

  • Tags

You can share this post!

Anavyovuna katika biashara ya kuchoma nyama  

Sonko aonyesha kamera za CCTV zilizosheheni kwake akisema...

T L