• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Mahakama yaambiwa Mackenzie aliongoza ibada za kuwazika waumini waliofunga wakaangamia

Mahakama yaambiwa Mackenzie aliongoza ibada za kuwazika waumini waliofunga wakaangamia

Na BRIAN OCHARO

MAHAKAMA ya Shanzu imeelezwa Ijumaa kuwa mhubiri Paul Mackenzie aliongoza hafla ya mazishi ya mamia ya wafuasi wake ambao walifariki baada ya kufunga kwa siku nyingi kwenye msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Stakabadhi zilizoletwa mahakamani zinaonyesha kuwa Mackenzie aliwasifu wale ambao walikuwa wakifa kama mashujaa na kuwashajiisha wale ambao bado walikuwa wakiendelea na mfungo wakaze kamba zaidi kwa kuwa ulimwengu ulikuwa unakaribia mwisho wake.

Kiongozi wa uchunguzi katika kesi inayomkabili Mackenzie katika Mahakama ya Uhakimu ya Mombasa Inspekta Raphael Wanjohi, amesema walipokea habari hizo kutoka kwa mashahidi ambao baadhi yao ni wale ambao waliokolewa kutoka kwenye msitu huo.

Mackenzie alikamatwa baada ya polisi kugundua kuwa kwenye ardhi ambayo inadaiwa kuwa ni yake katika msitu wa Shakahola, kulikuwa na makaburi ya halaiki. Pia anatuhumiwa kueneza mafundisho ya dini yenye ujumbe wa itikadi kali. Tayari miili 243 imeshafanyiwa upasuaji kubaini hasa kilichosababisha vifo vya wahanga wa Shakahola.

Serikali imeomba mahakama itoe uamuzi kuwa Mackenzie na baadhi ya wafuasi wake waendelee kuzuiliwa kwa siku 60 zaidi ila mawakili wa Mackenzie ambao ni Wycliffe Makasembo, Elisha Komora na George Kariuki wamepinga.

Mawakili hao wamesema polisi wamekuwa wakimzuilia mteja wao kwa mwezi mmoja na muda huo uliwatosha kumaliza uchunguzi wao.

Kesi hiyo itarejelewa Juni 7 ambapo utetezi wa Mackenzie utasikilizwa kabla ya hakimu kutangaza tarahe ambapo ataamua iwapo mhubiri huyo ataachiliwa kwa dhamana au kuzuiliwa kwa siku 60 zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wawili wauawa na Al-Shabaab katika Kaunti ya Mandera

Omtatah ataka vipengee tata 13 ving’olewe kwenye...

T L