• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Maina Njenga ahojiwa na DCI, polisi watawanya wafuasi wake

Maina Njenga ahojiwa na DCI, polisi watawanya wafuasi wake

NA STEVE OTIENO

MAAFISA wa polisi wamelazimika kuwatawanya wafuasi wa aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Bw Maina Njenga ambaye Alhamisi amefika katika makao makuu ya Idara ya Kupeleleza Makosa ya Jinai (DCI) ili kuhojiwa.

Mamia ya wafuasi wa Njenga walikuwa wamekita kambi nje ya lango la kuingia katika makao hayo ya DCI, Kiambu Road wakishinikiza kuachiliwa kwa Njenga.

Polisi wamelazimika kurusha gesi ya vitoa machozi kuwatawanya wafuasi wa Njenga waliotatiza shughuli kawaida katika barabara hiyo muhimu kwa magari yanayoingia jijini Nairobi kutoka Kiambu.

Viongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya wakiongozwa na kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na aliyekuwa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria wamefika katika makao makuu ya DCI.

Wamedai serikali ya Kenya Kwanza inamhangaisha Bw Njenga ili aachane na mrengo wa Azimio.

Bw Wamalwa amesema njama ya serikali haitafaulu.

“Hili ni swala la kisiasa. Wanataka kumlazimisha Maina Njenga ajiondoe katika mrengo wa Azimio aingie Kenya Kwanza,” amesema Bw Wamalwa ambaye ni kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K).

Naye Bw Kioni ameeleza jinsi maafisa wa DCI walivyomchukua mteja wao – Njenga – baada ya kuwadanganya mawakili kwamba walitaka aende pembeni washauriane kiasi.

“Tumekuwa mawakili sita tukizungumza na mteja wetu na ghafla maafisa wakatudanganya walitaka wazungumze naye pembeni ambapo wamemwondoa na kisha kufunga lango kubwa. Hatujui wamempeleka wapi,” amesema Kioni.

Amedai kwamba serikali imeona wapinzani kutoka eneo la Mlima Kenya wanazungumza kwa sauti moja na ni tishio kwa viongozi walioko madarakani.

  • Tags

You can share this post!

Microsoft ADC yashirikiana na YALI kuwahami vijana na ujuzi

Ashtakiwa kwa kutumia magari ya watu kuchukua mikopo

T L