• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Maiti ya ajuza aliyefariki 2004 hatimaye yazikwa

Maiti ya ajuza aliyefariki 2004 hatimaye yazikwa

Na PIUS MAUNDU

MAITI ya ajuza mmoja aliyefariki 17 iliyopita ilizikwa Jumamosi katika kijiji cha Mbusyani, Kaunti ya Machakos katika hafla fupi iliyotamatisha juhudi za familia yake za kutaka kumpa heshima za mwisho kwa taadhima.

Ilikuwa ni siku ya furaha kwa familia, jamaa, marafiki na majirani wa marehemu Esther Nzakwa Kitivo ambaye mazishi yake yalikwamishwa mnamo 2004 na mzozo kuhusu ardhi alikopangiwa kuzikwa.

“Tunashukuru Mungu kwa kumpa mama yetu miaka 93 maishani na miaka mingine 17 katika kifo,” Bw Michael Kitivo, mwana wa kiume wa mwendazake, akasema kwenye hotuba yake wakati wa mazishi hayo.

Nzakwa alifariki mnamo Agosti 31, 2004, baada ya kuugua maradhi ya pumu na maradhi mengine yanayohusiana na uzee.

Lakini hakuzikwa siku chache baadaye kutokana na mvutano kuhusu kipande kimoja cha ardhi.

Marehemu, ambaye alikuwa mke wa kwanza wa marehemu Gideon Kitivo ambaye pia alikuwa na wake wengine wawili, alikuwa ametambua sehemu fulani ya ardhi ya familia kama yake.

Kulingana na watu wa familia, hapo ndipo alipotaka azikwe atakapofariki.

Lakini hakufahamu kuwa wengine katika familia hiyo walikuwa na mipango tofauti.

Mipango ya kumzika Nzakwa mnamo 2004 ilikatizwa baada ya mmoja wa wanawe wa kambo pia kudai umiliki wa ardhi hiyo ambako alipangiwa kuzikwa.

Baada ya kupata kibali kutoka kwa Bodi ya Kusimamia Ardhi, Bw Morris Kitivo alienda mahakamani na kupata agizo la kusimamisha mazishi ya mama yake huyo wa kambo katika kipande hicho cha ardhi.

Kesi hiyo iliendelea mahakamani kwa muda mrefu na kufikia 2014 ilikuwa imeshughulikiwa na majaji saba wa Mahakama Kuu.

Lakini hadi sasa mahakama kuu haijatoa uamuzi kuhusu kesi hiyo.

Msukumo kutoka kwa familia ikitaka maiti ya Mama Nzakwa izikwe ulisababisha Bw Michael Kitivo, ambaye ni mwanawe, kukubali mazishi yafanywe katika boma lake wakisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu kesi iliyowasilishwa na kaka yake wa kambo.

You can share this post!

Watford wakomoa Millwall na kupanda ngazi kushiriki Ligi...

KEMSA: Murathe apanga kujitetea mbele ya kamati