Serikali sasa imepata majina ya watoto 131 waliofariki katika mfungo hatari huko Shakahola, uliosababisha vifo vya waumini zaidi ya 400 wa Kanisa la Good News International.
Mahakama ya Shanzu ilisikia Jumatatu kwamba wachunguzi wamepata majina 131 kati ya watoto 184 walioangamia katika msitu huo mkubwa.
“Kilichosalia kwa sasa ni kuoanishwa kwa majina na miili iliyo katika chumba cha kuhifadhia maiti,” Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma Jami Yamina alisema.
Bw Yamina alimweleza Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Shanzu Yusuf Shikanda kwamba ingawa stakabadhi za watoto hao ziliharibiwa, wachunguzi wamefaulu kuunganisha ushahidi na sasa wana uhakika kwamba maelezo muhimu yamepatikana.
Alieleza zaidi kuwa wachunguzi hao wanahitaji muda zaidi wa kuoanisha kwa usahihi kila jina na maiti yake , ambayo kwa sasa inahifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya Malindi.
“Watoto wote 131 wanauhusiano wa karibu na washtakiwa 30 katika kesi hii na wale manusura 66. Tunayo majina sasa kwa ajili ya kutayarisha mashtaka dhidi ya washtakiwa. Hata hivyo, tunafaa kubaini ni jina gani linalolingana na maiti ipi ,” Bw Yamina alisema.
Kiongozi huyo wa mashtaka alisema majina ya watoto waliofariki yalipowasilishwa kwa manusura 66 mahakamani mapema mwezi huu, hawakujibu wala kukanusha ushahidi huo.
“Badala yake, manusura hao waliambia serikali itoa ushahidi kwamba watoto hao hawako mbinguni, kutokana na uthibitisho wa vifo vyao,” mwendesha mashtaka alisema.
Zaidi ya hayo, ripoti ya uchunguzi wa kijamii imependekeza kuwa ni wafuasi sita pekee wa Paul Mackenzie wanaweza kuachiliwa kwa dhamana huku wakisubiri kufunguliwa mashtaka rasmi na kesi yao kusikilizwa.
Hata hivyo, serikali imesema kuwa ushahidi uliokusanywa hadi sasa unaonyesha kuwa hakuna mshukiwa yeyote anayepaswa kuachiliwa kwa dhamana kabla au baada ya kufunguliwa mashtaka rasmi.
“Wakati mahakama inazingatia iwapo watu hao sita wanaweza kuachiliwa kwa dhamana, msimamo wetu ni kwamba kulingana na ushahidi uliotolewa, wao ni wafuasi wa kanisa la Good News International na bado wanashikilia imani yake. Mapendekezo zaidi ya kuachiliwa kwao kwa dhamana hayapunguzi ushahidi wa kuhusika kwao katika mauaji ya Shakahola,” akasema Bw Yamina.
Mwendesha mashtaka alifichua kwamba serikali tayari ina nia ya kuwafungulia watu hao mashtaka ya itikadi kali, mauaji bila kusudia na mauaji.
“Sio makosa yote yatahitaji kutambuliwa kwa wahasiriwa. Kuna ushahidi wa kutosha wa kuleta mashtaka ya itikadi kali. Wanaweza kushtakiwa kwa kosa hili kama waasi au waendelezaji wa imani kali,” alisema.
Hata hivyo, wakili wa watuhumiwa hao, Bw Wycliffe Makasembo, aliiomba mahakama iwaachie huru huku akieleza kuwa serikali haijawasilisha ushahidi mpya wa kuendelea kuzuiliwa.
Kulingana na wakili huyo, hakuna ushahidi mpya unayoweza kuainishwa kuwa ya dharura ili kuwanyima watu hao dhamana au kuendelea kuzuiliwa tena kwa siku 180.
“Ombi hili ni sawa na asilimia 100 ya maombi mengine yote ya awali ambayo yamejadiliwa mbele ya mahakama hii. Mahakama imeamua kuhusu maombi haya . Tunaiomba mahakama ikatae ombi hili na kuwakubali washtakiwa waachiliwe wa dhamana huku wakisubiri kufunguliwa mashtaka rasmi,” alisema.
Bw Makasembo amesema kuwa madai ya serikali hayajaungwa mkono na ushahidi wowote bali yamejaa uvumi tu.
Wakili huyo amelalamika kwamba ombi la serikali linatokana na uvumi, hofu za uwongo na madai ambayo hayawezi kuwa msingi wa kuendelea kuzuiliwa kwa wateja wake.