• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
Makundi sasa kupata mkopo wa Hasla

Makundi sasa kupata mkopo wa Hasla

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto mnamo Alhamisi alizindua huduma nyingine ya mpango wa utoaji mikopo kutoka kwa Hazina ya Hasla unaolenga makundi yaliyosajiliwa.

Dkt Ruto alifanya uzinduzi huo katika uwanja wa Moi mjini Embu ambako aliongoza sherehe za 60 za Sikukuu ya Madaraka Dei.

“Ni furaha yangu kutangaza wakati wa sherehe za leo (jana Alhamisi) kwamba baada ya hotuba yangu nitazindua huduma myingine ya Hazina ya Hasla itakayowawezesha watu kupata mikopo kupitia makundi,” akasema.

Rais alisema kupitia huduma hiyo makundi kama vile makundi ya kujisaidia (chama) na mashirika ya akiba na mikopo (saccos) yatapewa mikopo ya kuanzia Sh20,000 hadi Sh1 milioni. Mkopo huo utatozwa riba ya asilimia saba (7) kila mwaka.

“Mikopo hii itawezesha makundi haya kushiriki kikamilifu katika shughuli za utoaji mikopo kwa wanachama, kuweka, kuanzisha hazina ya uzee, kulipia bima ya matibabu miongoni mwa huduma nyinginezo,” akasema Dkt Ruto.

“Sasa ni fahari yangu kuanzisha huduma ya Mkopo wa Makundi chini ya Hazina ya Hasla. Naamini kuwa hii ni habari njema kwa rafiki yangu Shiko kutoka Ruaka,” akaongeza.

Dkt Ruto alisema kuwa mkopo wa Hazina ya Hasla unapatikana kwa haraka kupitia simu ya mkononi ambayo ndio njia bora akihimiza Wakenya kutatumia ubunifu wa kiteknolojia kuboresha maisha yao.

Rais alisema serikali yake imejitolea kufaidi kutokana na teknolojia ya kifedha kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma kwenye mpango wa ustawishaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.

Kiongozi wa taifa alisema kuwa kufikia sasa jumla ya Wakenya 20.2 milioni wamepokea mkopo wa Sh30 bilioni kutoka kwa Hazina ya Hasla na kulipa jumla Sh19.7 bilioni.

Wakenya milioni 7 wamekopa na kulipa pesa hizo zaidi ya mara moja.

“Hakuna pesa zimeibiwa kupitia ufisadi, na wakopaji hawahitaji kumjua mtu yeyote, kumhonga afisa yeyoye au kupitia taratibu ndefu kupata mkopo wa Hazina ya Hasla. Wanachohitaji ni simu, mjazo na dakika chache na wanaweza kupata pesa popote walipo,” Dkt Ruto akasema.

  • Tags

You can share this post!

Matano asema Tusker hawana mpango wa kumsajili Lewis Bandi...

Chuo Kikuu cha Mtandaoni kuzinduliwa rasmi mwezi huu,...

T L