• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Mamia wafutwa kazi katika kiwanda cha kahawa mikakati ya Gachagua ikiibua maswali

Mamia wafutwa kazi katika kiwanda cha kahawa mikakati ya Gachagua ikiibua maswali

NA STEPHEN MUNYIRI

WAFANYAKAZI wapatao 400 wa kiwanda cha kahawa walifutwa kazi Jumatatu kufuatia hatua ya serikali ya kukatiza mkataba wa kampuni iliyokuwa imewaaajiri kusaga na kuuza kahawa.

Haya yamejiri huku athari za mageuzi katika sekta ya kilimo cha kahawa yanayoongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua zikianza kujitokeza katika ngome yake binafsi.

Waajiriwa wa Kampuni ya Kusaga Kahawa ya Central Kenya katika eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri, walipigwa na butwaa walipofika kazini kama kawaida mnamo Jumatatu na kukabidhiwa barua za kuwaachisha kazi.

Mamia ya wawekezaji karibu na kiwanda hicho vilevile wamekumbwa na wasiwasi wakihofia kupata hasara ya mamilioni hasa wastawishaji waliokuwa wamejenga makazi ya kupangisha.

Hatua ya kufunga kiwanda hicho imewakatiza tamaa maelfu ya wakulima wa kahawa mjini Mathira na maeneo mengine jirani wanaosema kiwanda hicho kilichokuwa karibu kiliwapa afueni kuhusiana na gharama za usafirishaji.

Walioathirika pia ni mamia ya wamiliki duka, wachuuzi wa vyakula, wauzaji bidhaa, mamia ya vibarua miongoni mwa wengine wanaonufaika moja kwa moja kutokana na kiwanda hicho kilichopo mashinani.

Udadisi uliofanywa na Taifa Leo Jumatano katika kiwanda hicho kilichopo Mathaithi umbali wa karibu kilomita tatu kutoka Karatina, ulibainisha kuwa kituo hicho kilichofunguliwa mnamo 2004, kilifunga operesheni zake ambapo usimamizi uliwakabidhi waajiriwa barua za kuwaachisha kazi mnamo Desemba 4, 2023.

Kiwanda hicho ambacho ndicho pekee kinachotoa huduma za kusaga kahawa eneo hilo, kimekuwa kikiunda na kuuza kahawa kutoka Kaunti za Nyeri, Murang’a, Kirinyaga, Embu na Meru.

Nakala ya barua za kuachishwa kazi zilizoonekana na Taifa Leo ambazo zilizandikwa Desemba 4 na kutiwa saini na mkurugenzi aliyehudumu kwa miaka mingi, Charles Mwea, zinaashiria kwamba wafanyakazi wote walikuwa wamepatiwa notisi ya kuwafuta kazi mnamo Novemba 29.

“Tunarejelea barua iliyoandikwa Novemba 29, 2023, iliyowapa notisi kuhusu nia ya kukatiza mkataba wenu wa ajira. Hivyo basi tunakatiza kandarasi yenu ya ajira na Kiwanda cha Kusaga Kahawa cha Central Kenya kuanzia Desemba 31, 2023,” ilisema barua hiyo.

Kulingana na barua hiyo, waajiriwa watalipwa mishahara yao na marupurupu mengineyo ya hadi Desemba 31 mwaka huu.

Naibu Rais ameanzisha kampeni kali ya mageuzi katika sekta ya kahawa baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto kupitia Amri ya Rais kuongoza kinachofahamika kwa sasa kama “Mageuzi ya Rigathi.”

Hata hivyo, kampeni yake imeonekana kukinzana na matokeo huku mauzo kwenye Soko la Hisa la Nairobi yakiporomoka na kuwaacha wakulima wakilalamikia kupata hasara kuhusiana na bei.

Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na Taifa Leo kwa faragha walisema japo wamevunjwa moyo na barua hizo za kuwaachisha kazi, hawakushtuka sana kwa sababu walikuwa wamefahamu awali mwajiri wao alinyimwa leseni.

  • Tags

You can share this post!

Aliuza mbuzi wake kupata pesa za Krismasi, lakini jambazi...

Mwanawe Rais atupwa rumande baada ya kukanyaga mtu...

T L